Kenya yawaonya watumiaji wa mitandao ya kijamii
17 Julai 2017Huku zikiwa zimesalia siku 20 kabla ya uchaguzi mkuu nchini kenya, wakenya wa matabaka mbali mbali wana wasiwasi hasa kuhusu joto la siasa linaloendelea kupanda kwenye mitandao ya kijamii.
Kwenye mkutano na wadau wanaohusika na maandalizi ya uchaguzi mkuu, Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya mawasiliano nchini Kenya Francis Wangusi alionya kuwa mitandao inayochapisha habari za uzushi itafungwa.
Mwenyekiti wa tume ya uwiano na utangamano Francis Ole Kaparo kwa upande wake alisema kuwa wanachunguza wasimamizi wa mitandao ya WhatsApp 21 ambayo imekuwa ikichapisha taarifa za uzushi na kwamba uchunguzi unaendelea. Hayo yanajiri siku chache tu baada ya baadhi ya mitandao kuchapisha taarifa za uzushi kuwa rais mstaafu Mwai Kibaki ameaga dunia.
Wakati hayo yakijiri nchini Kenya, shirika la utafiti la Paradigm Initiative Nigeria, limetoa matokeo ya utafiti wake unaoonyesha kuwa kuwa mataifa ya Afrika Mashariki ni miongoni mwa mataifa yanayoongoza kwa ukiukaji wa uhuru wa kujieleza kwenye mitandao ya kijamii.
Dola milioni 5.8 kutumika kuchunguza watumiaji
Ni kutokana na hilo ambapo sekta binafasi nchini Kenya iliwaleta pamoja wadau wanaoandaa uchaguzi kuwahakikishia wawekezaji usalama wao. Serikali imesema kuwa haitakubali watumiaji wa mitandao kuvuruga amani kwa kueneza habari za uzushi.
"Waambie wakenya, hakuna mahali wanaweza kujificha hata kwenye mitandao ya kijamii bila ya kutambuliwa. Hatufikirii kufunga mtandao wa inteneti kama vile watu wanavyosema,” alisema Francis Wangusi, mkurugenzi wa mamlaka ya mawasiliano nchini Kenya, CAK.
Serikali imewekeza dola milioni 5.8 sawa na shilingi milioni 600 za kuchunguza wanaotumia mitandao ya kijamii kwa njia isiyostahili. Wangusi alivionya vyombo vya habari dhidi ya kutangaza matokeo ya uchaguzi kabla ya tume ya kusimamia uchaguzi na mipaka kufanya hivyo.
Wasimamizi wa mitandao ya WhatsApp wameonywa dhidi ya kupeperusha habari za uvumi, hata hivyo kulingana na wachambuzi, hatua ya kuwapata wachochezi hao itakuwa vigumu, kwa kuzingatia historia mbovu ya taifa hilo ya kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaohusika na uchochezi wa mitandaoni.
Lakini Francis Ole Kaparo, mwenyekiti wa tume ya uwiano na utangamano nchini Kenya, anasema wamezitambua "Group" 21 za WhatsApp ambazo zinaeneza chuki na uchochezi kote nchini na wanaendeela kuwachunguza wasimamizi wa group hizo. "Njia bora za kukabili suala hilo ni kuwatafuta wasimamizi wa mitandao hiyo,” alisema Kaparo.
Polisi kutumia nguvu kukabiliana na maandamano
Kwa upande wa vyombo vya usalama, inspekta jenerali wa polisi Joseph Boinet amesema polisi watatumia nguvu kiasi kuwakabili wachochezi wa ghasia iwapo fujo zitazuka. Onyo lake linakumbusha matukio ya mwaka 2007/08 wakati polisi walipotuhumiwa kuhusika na mauaji ya kiholela walipokuwa wakikabiliana na ghasia.
Inakadiriwa watu 1133 waliuawa huku wengine nusu milioni wakipoteza makazi katika machafuko hayo ambayo hadi wakati huu wahusika wake walishindwa kuchukuliwa hatua zozote, na juhudi za mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC kufungua mashitaka ziligonga mwamba.
Kaimu waziri wa usalama wa taifa Fred Mataingi akitilia mkazo juhudi za serikali za kuhakikisha uchaguzi huru na haki, amewaonya kuwaonya wanaovunja sheria kwa kutumia mitandao ya kijamii kwa kusema: "Tutahakikisha kuwa sheria inazingatiwa bila ya kubagua na tutasimama imara”.
Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 69 ya Wakenya wanatumia mitandao ya kijamii, huku wale wanaotumia simu ikifikia asilimia 74. Serikali nyingi barani Afrika zinafunga mitandao ya kijamii kwa hofu ya watumiaji kueneza uchochezi kwa kufunga mitandao kama ilivyotokea nchini Ethiopia, Uganda na Burundi. Huku Kenya, Tanzania na Rwanda zikiweka sheria kali za kuwadhibiti wanaochochea na kueneza habari za uwongo kwenye mitandao.
Mwandishi: Shisia Wassilwa
Mhariri: Saumu Yusuf