Kenya yawazuia raia wake kujiunga na vita vya Ukraine
17 Machi 2026
Wakenya wamekuwa na hisia mbali mbali baada ya Serikali ya taifa hilo kutangaza kuwa raia wa taifa hilo hawataruhusiwa tena kujiunga na jeshi la Urusi kupigana katika vita vya Ukraine, kufuatia makubaliano mapya kati ya nchi hizo mbili.
Waziri wa Masuala ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, alisema uamuzi huo ulifikiwa baada ya mazungumzo na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, mjini Moscow. Wakenya 1000 wanapigana kwenye vita hivyo dhidi ya Ukraine.
Hatua hiyo ilichukuliwa kufuatia shinikizo kubwa kutoka kwa familia na umma nchini Kenya, baada ya kubainika kuwa zaidi ya Wakenya 1,000 walikuwa wamejiunga au kupelekwa kupigana vitani, wengi wao wakivutwa na ahadi za mishahara mikubwa na marupurupu.
Mudavadi: Serikali kushughulikia ustawi wa Wakenya walioko Urusi
Ripoti pia zimeonyesha kuwa baadhi ya waajiri walikuwa wakitumia udanganyifu, wakiahidi ajira za kiraia lakini baadaye kuwapeleka waathiriwa kwenye mapambano ya mstari wa mbele nchini Ukraine. Waziri Mudavadi alibainisha kuwa serikali ya Kenya sasa itashughulikia ustawi wa Wakenya walioko Urusi kupitia njia rasmi za kidiplomasia, ikiwa ni pamoja na huduma za ubalozi.
Kwenye kikao hicho kilichofanyika Moscow Kenya na Urusi zimekubaliana kuhusu kurejeshwa salama kwa raia wa Kenya waliokuwa wakihusika katika operesheni za kijeshi za Urusi, pamoja na kulipwa fidia kwa wale waliojeruhiwa na familia za wale waliopoteza maisha. Hizi hapa hisia za Wakenya kuhusu uamuzi huo.
Kenya ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yaliyokumbwa na tatizo hilo, huku mataifa kama Ghana na Afrika Kusini yakiripoti visa vya raia wao kushawishiwa au kudanganywa kujiunga na vita hivyo.
Makubaliano mapya kati ya Nairobi na Moscow
Uamuzi huu unaashiria hatua muhimu ya serikali ya Kenya kulinda raia wake dhidi ya ushiriki katika migogoro ya kigeni, huku pia ukidumisha uhusiano wa kidiplomasia na Urusi katika sekta nyingine kama biashara, nishati na utalii.
Kwa upana zaidi, kisa hiki kinaakisi tatizo la kimfumo linaloikumba Afrika na dunia kwa jumla, ambapo ukosefu wa ajira na fursa unasukuma vijana kuingia katika mitego ya ajira zisizoeleweka, ambazo wakati mwingine huishia kuwa hatari kwa maisha yao.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari Mudavadi alisema suala hilo lilijadiliwa wakati wa mazungumzo rasmi ya pande mbili na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov. Chekai Musa ni mchambuzi wa masuala ya kimataifa.
"suala kuu linalowasukuma vijana kuenda nje ya taifa ni kwa sababu hawana ajira, je ni suluhisho gani Mudavadi amewapa mamilioni ya vijana ambao hawana ajira? Urusi ingali inatafuta vijana kutoka Uganda na mataifa mengine kupigia Urusi.”
Serikali hizo mbili pia zilijadili kukamilisha makubaliano ya kuanzisha Tume ya Kiserikali ya Ushirikiano wa Kiuchumi, ambayo itatoa mfumo rasmi wa kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Shisia Wasilwa, Dw Nairobi