Kenya yazindua kamati maalum kushughulikia ukame
25 Novemba 2022Wakati huo huo, operesheni za kugawa chakula cha msaada zinaendelea kote nchini humo wakati huu wakaazi wa kaunti 20 wakipambana na njaa kali na ukame hasa kwenye maeneo ambayo hupata mvua kidogo.
Kenya kushirikiana na Israel kiteknolojia katika kilimo
Kamati hiyo ya utendaji itahudumu kwa mwaka mmoja chini ya ofisi ya naibu wa rais. Kwenye uzinduzi rasmi, naibu wa rais Rigathi Gachagua aliwatahadharisha matapeli na wahuni juu ya wizi wa hela za ufadhili wa njaa na madhila ya ukame.
Mwanzoni mwa wiki hii, Rigathi Gachagua alilizuru eneo la Garissa ambayo ni moja ya kaunti 11 zilizo katika hali mbaya ya ukame na njaa.
Kamati hiyo ya utendaji inasimamiwa na afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom, Peter Ndegwa.
Mataifa kame yaunda muungano kukabiliana na uhaba wa maji
Kikosi hicho kinawaleta pamoja maafisa watendaji wa sekta za umma na binafsi kushirikiana ili kuchangisha hela kuzipa msukumo juhudi za serikali kuu na shirika la Msalaba Mwekundu za kupambana na njaa.
Hela zote zitaelekezwa kwenye mkondo mmoja kupitia nambari maalum ya malipo ya simu za mkononi.
Ifahamike kuwa jumla ya kaunti 20 zinaandamwa na ukame na njaa kali. Hali ni mbaya katika kaunti 11 ambazo ni Turkana, Samburu, Tana River, Marsabit, Wajir, Mandera, Kitui, Garissa, Kajiado, Laikipia na Isiolo.
Mvua zimekosa kunyesha katika baadhi ya maeneo ya Kenya kwa misimu minne iliyopita na inayonyesha kwa sasa ni chache na ilianza kwa kuchelewa.
Hali hiyo ya hewa imesababisha mambo kuwa magumu kwenye wadi 45 za ziada zilizoko kaunti 9 ambazo kwa kawaida hazitatizwi na ukame.
Hali hii inaarifiwa kuongeza migogoro baina ya jamii za wafugaji. Abdi Ibrahim Guyo ambaye ni gavana wa Isiolo na amekiri kuwa ukame upo ila kudumisha amani kati ya wafugaji ni muhimu.
Haya yanajiri wakati kaunti za Meru, Tharaka-Nithi, Embu, Nyeri, Kilifi, Kwale, Taita-Taveta, Makueni na Narok ziko katika hali ya tahadhari.
Mwandishi: Thelma Mwadzaya, DW Nairobi