1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yazindua mpango wa kuuza mifugo nje ya nchi

Thelma Mwadzaya28 Oktoba 2022

Ukame umewaua ngombe milioni 2.5 katika maeneo yanayokabiliana na uhaba wa mvua nchini Kenya.Ili kunusuru hali, serikali imezindua mpango wa kuuza nje mifugo na tayari shehena ya kwanza iko njiani kuelekea Oman.

Kenia Dürre in Samburu
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Akizungumza kwenye warsha ya kisayansi iliyoandaliwa na chama cha wafugaji ,APSK, Katibu wa wizara ya mifugo Harry Kimutai alibainisha kuwa wanyama wapo ila wako hali mbaya kiafya kwasababu ya ukame.

Kwa upande wake, serikali ya Kenya inajitahidi kuingilia kati kuwanusuru wafugaji kwa kuwashawishi wauze wanyama wao kwa mataifa ya mashariki ya kati.

Mfugaji akiwa katikati ya mifugo yake iliyokufa huko Marsabit KenyaPicha: BAZ RATNER/REUTERS

Oman imeingia ubia na serikali ya Kenya kununua mifugo iliyo hai. Wiki iliyopita, shehena ya kila mwezi ya mifugo ilianza safari yake kuelekea Oman. Kupitia meli kwa jina MV Banyas 1, ng'ombe madume  200,mbuzi na kondoo 11,200 walisafirishwa kutokea bandari ya Lamu.

Ukame umeathiri hali katika kaunti 29 ambazo sasa zinakabiliana na uhaba mkubwa wa maji na nyasi za malisho.Kwa sasa mpango huo wa kununua mifugo kutokea maeneo yanayotatizwa na ukame unazishirikisha kaunti 14.

Kadhalika upo mpango mwengine wa kuwawezesha wafugaji kuimarisha biashara uanojikita katika lishe bora la wanyama na kusaka soko la bidhaa za nyama na maziwa.

Mpango huo wa miaka mitano unasimamiwa na shirika la misaada la Marekani,USAID, kwa ushirikiano na wizara ya mifugo ya Kenya.

Kampuni ya Al Bashayer iliyoko Oman ndiyo inayonunua mifugo kutokea maeneo yanayotatizwa na ukame.Mifugo hiyo ilisafirishwa kutokea bandari ya Lamu kuelekea Salalah.

Kwa sasa ina sehemu ya ardhi mkabala na bandari hiyo ya Lamu inayotumika kuwahifadhi wanyama ili wafanyiwe ukaguzi wa kiafya kabla ya kusafirishwa. Juma Mwadunje ni afisa wa afya kwenye bandari ya Lamu na anaelezea tahadhari wanazochukua kwenye meli.

Ng'ombe aliyedhoofika kwasababu katika kaunti ya Wajir KenyaPicha: Ed Ram/Getty Images

Bandari ya Lamu itakuwa na uwezo wa kutumika kusafirisha mifugo laki tatu kwa mwaka mradi utakaposhika kasi.Hii ni mara ya kwanza kwa mifugo kusafirishwa kutokea Lamu ila ni shehena ya tatu kutoka Kenya kwa mwaka huu.Shehena ya kwanza na ya pili ilisafirishwa kutokea bandari ya Mombasa.Ukame Pembe ya Afrika wasababisha njaa kwa watu milioni 13

Safari ya meli kutokea Lamu hadi Salalah inachukua wiki moja ikiwa bahari imetulia.Kampuni ya Al Bashayer inatumia meli kwa jina Banyas 1 iliyo na asili ya Togo itakuwa ikitia nanga Lamu kwa mwaka mmoja.Bandari ya Lamu ilianza operesheni zake Mei mwaka uliopita na kufikia sasa meli 13 zimeitumia.

Mifugo inayouzwa nje hutokea maeneo ya Garissa wanakofugwa mbuzi aina ya Galla wanaoweza kuhimili magonjwa katika maeneo ya yasiyokuwa ya milimani. Ngombe nao hutokea kaunti ya Laikipia na kondoo aina ya merino wanapatikana Narok huku ngamia wakitokea Tana River.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW