Kenya yazindua utoaji chanjo dhidi ya covid-19
5 Machi 2021Dozi millioni 1.02 za chanjo ya virusi vya corona ziliwasili siku ya Jumanne, na kuwa moja ya mataifa ya mwanzo kupokea chanjo hiyo barani Afrika.
Zoezi hilo muhimu lilizinduliwa kwenye hospitali kuu ya Kenyatta hapa jijini Nairobi. Pamoja na wahudumu wa afya, wengine watakaochanjwa katika awamu hii ya kwanza ni pamoja na maafisa wa usalama, walimu na watu wazima walio na umri wa miaka 50 na zaidi. Katibu mkuu wa wizara ya afya nchini Kenya Susan Mochache amesema haya walipoanza kugawa chanjo hiyo mpya.
"chanjo itaanza kwa wale wanaofanya kazi mahospitalini, wauguzi, madaktari, tumeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba kaunti zote zitapata vaccine(chanjo) na baada ya mwezi wa tano tutaanza kuangazia wale ambao wamefika miaka 50 kwenda juu na wale ambao wana ugonjwa mwilini ambao inapaswa wapewe chanjo ili ugonjwa huu wa COVID usiwaangamize", alisema Mochache.
Soma Zaidi: Majaribio ya chanjo ya COVID-19 yaidhinishwa Kenya
Kufikia sasa dozi laki 490 zimeshasafirishwa hadi vituo maalum vya kuhifadhi chanjo kote nchini. Hospitali za daraja la juu zaidi zitapokea dozi alfu 33, na zile za jeshi zimetengewa alfu 21. Azma ya kufuata mpangilio huu ni kuwazuwia watundu na Walio na ubinafsi kujiweka mstari wa mbele na kupokea chanjo. Dr Patrick Amoth ni mkurugenzi mkuu wa wizara ya afya nchini Kenya na ndiye aliyekuwa wa kwanza kupokea chanjo hiyo asubuhi hii.
"Najua ya kwamba hii process(mchakato) waliotumia kutengeneza hii chanjo ni mchakato ambao umahekikiwa kabisa na nawahimiza Wakenya wenzetu wajitokeze ukifika ule wakati na ninawahakikishia kwamba mimi mwenyewe nimesimama hapa nimechanjwa" alinukuliwa Dr. Amoth.
Ifahamike kuwa chanjo hiyo mpya ilianza kusambazwa rasmi saa Chache zilizopita. Baadhi wanatiwa hofu na athari za chanjo hiyo ingawa Dr Bernard Ogutu ni mtaalam wa utafiti wa chanjo na dawa Katika taasisi ya utafiti wa tiba KEMRI ana mtizamo chanya kuhusu chanjo hiyo.
Akizindua rasmi shughuli hiyo eneo la kuhufadhia chanjo la Kitengela,Rais Uhuru Kenyatta alisisitiza kuwa huu ni mwanzo wa Safari ndefu ya kupambana na COVID 19 ana kwa ana.
Rais Uhuru Kenyatta aliweka bayana kuwa dozi za ziada za chanjo ya COVID 19 zinatarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa Aprili mwaka huu.
Kwa upande wa pili magavana wameelezea wasiwasi wao mintarafu mpangiliio wa kugawa na kuwachanja wakenya. Serikali za kaunti zina wajibu wa kuhakikisha kuwa chanjo hizo zinahifadhiwa kwa njia mujarab ukizingatia nguvu za umeme za kuaminika. Kisayansi sharti zihifadhiwe kwenye mazingira ya nyuzi joto Kati ya -15 na 25 ndipo ziweze kufanya kazi.
Soma Zaidi: COVID-19 ni mtihani mkubwa kwa Wakenya kujikimu kimaisha
Thelma Mwadzaya- Nairobi