1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yazuia wanariadha kushiriki mashindano ya kimataifa

Deo Kaji Makomba
12 Machi 2020

Kenya imewazuia wanariadha wake kushiriki mashindano ya kimataifa kufuatia hofu ya kusambaa kwa virusi hatari vya Corona ambavyo vimesababisha wasiwasi mkubwa duniani. Chimbuko lake ni katika mji wa Wuhan nchini China.

Kenyan Athlet Vincent Kipruto
Mwanariadha wa Kenya Vincent KiprutoPicha: picture-alliance/dpa/E. Naranjo

Katazo hilo kwa wanariadha wa Kenya limetolewa Alhamisi hii na Shirikisho la riadha nchini humo kwa kuwazuia wanariadha wake kusafiri nje ya nchi hiyo kwa ajili ya kushiriki mashindano ya riadha ya kimataifa kufuatia mlipuko wa virusi vya corona. Tangazo hilo limekuja siku moja tu mara baada ya Shirika la afya duniani WHO, kutangaza kuwa mlipuko wa virusi vya corona ni janga la kimataifa.

Kulingana na taarifa rasmi iliyotolewa na shirika la habari la Reuters, zaidi ya watu 126,000 duniani wameathirika na virusi hivyo na wengine zaidi ya 4,600 wamefariki dunia.

Nchi hiyo ya ukanda wa Afrika Mashariki ambayo haina kisa kilichothibitishwa kuhusiana na virusi hivyo vya corona imekuwa ikitoa baadhi ya wanariadha wa viwango vya juu duniani ambao mara kwa mara wamekuwa wakishinda medali mbalimbali katika mashindano ya kimataifa katika bara la Ulaya, Asia na Amerika ya Kaskazini.

"Kufuatia maelekezo kutoka katika serikali ya Kenya na kutokana virusi vya COVID 19 kuwa ni janga la kimataifa, Shirikisho la riadha nchini Kenya limesimamisaha safari zote za wanariadha katika mashindano ya kimataifa." Limesema shirikisho hilo katika taarifa yake na kuongeza kuwa limefanya hivyo kwa lengo la kulinda usalama wa wanariadha hao halikadhalika nchi ya Kenya kutokana na virusi hivyo. "Tunatoa wito kwa wanariadha kufuta mipango ya safari zao kwa mwezi ujao hadi pale taarifa zaidi zitakapotolewa."

Kenya imekuwa ikitoa wanariadha mahiri katika ulingo wa kimataifa

Rais Uhuru Kenyata akisalimiana na wanariadha wa KenyaPicha: Reuters/T. Mukoya

Akizungumza na shirika la habari la habari la Reuters, Benard Ouma ambaye ni mkufunzi wa mwanariadha wa kimataifa wa mbio za mita 1,500, Timothy Cheruiyot, amesema kuwa kwa pamoja wamechukua tahadhari kama serikali ya Kenya ilivyochukua tahadhari.

"Hatari ya kueneza virusi hivyo ndio tunajaribu kuepukana nayo. Hivyo hatua zinazochukuliwa na mamlaka tutakubaliana nazo. Mwisho wa siku ni suala la afya...kama kusafiri kunaweza kupelekea kuugua, basi yakupasa kuepuka safari." Amesema Ouma.

Wenyeji wa matukio ya kimichezo katika sehemu mbalimbali duniani wamefuta au kuahirisha matukio hayo kwa kuzuia mikusanyiko ya watu, ikiwa ni hatua za nchi husika kupambana na kuenea kwa virusi hivyo hatari vilivyokwishakuua maelfu ya watu huku wengine wakiathirika katika nchi mbalimbali duniani.

 

Chanzo: Reuters

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW