1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya:Kongamano lajadili maendeleo kwa maeneo yaliosahaulika

Eric Ponda6 Septemba 2018

Kongamano la viongozi kutoka sehemu zilizokumbwa na ukame na zile zisizotumika kikamilifu nchini Kenya limefanyika Malindi kujadili mkakati kuhusu maendeleo kwa sehemu hizo zilizosahaulika tangu Kenya ipate uhuru wake.

ASAL conference participants
Kutoka kushoto: Katibu mkuu wa wizara ya ugatuzi Eugene Wamalwa, gavana wa kauti ya Kilifi Amason Kingi, Naibu Rais William Ruto na gavana wa Turkana Josephat Nanok, wakifungua mkutano huo, Septemba 6, 2018.Picha: DW/E. Ponda

Maeneo yanayolengwa na mkutano huo wa siku tatu ulioanza siku ya Jumatano, ni yale yanayokaliwa na jamii za wafugaji wa kuhamahama, mfano kaskazini mashariki mwa Kenya katika mpaka na nchi jirani ya Somalia, majimbo ya Marsabit, Turkana na baadhi ya maeneo ya pwani ambayo tayari yametajwa kuwa sehemu zilizoachwa nyuma kimaendeleo kwa kubaguliwa na serikali zilizopita tangu ukoloni.

Kwa muda wa miaka 50 ya uhuru wa Kenya, bado asilimia kubwa ya maendeleo katika maeneo haya ni kupitia ufadhili kutoka kwa washrika wa kigeni.

Hata hivyo akifungua rasmi kongamano hilo, Naibu wa Rais wa Kenya William Ruto aliwaomba radhi wakaazi wa maeneo haya kwa dhulma za kihistoria huku akiongeza kuwa historia itakuwa na  maana tu ikiwa itatumia kurekebisha makosa na kuwa  na muongozo kwa mabadiliko ya maendeleo.

Gavana Amason Kingi akimkaribisha balozi wa Marekani nchini Kenya Robert Godec.Picha: DW/E. Ponda

"Ili kubadilisha mtazamo wa kimaendeleo katika sehemu hizi kame, ni lazima tutafute mkakati mbadala wa kufufa uchumi pasi na kutegemea mgawo wa serikali kwa majimbo haya, na ile hazina maalum ya serikali kwa sehemu zinazokumbwa na hali ngumu kimazingira. Na ndio sababu tuko hapa kutafuta mbinu za kutumia kikamilifu rasilimali zilizopo kwa maendeleo endelevu katika sehemu hizi," alisema Ruto.

Ili Kuupiga jeki ukuaji wa uchumi wa maeneo haya, mnamo mwaka wa 2014 Serikali ya Kenya ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 12 katika bajeti yake ili kuharakisha miradi ya maendeleo katika sehemu hizi, ingawa fedha hizo bado hazijaanza kutumika licha ya kwamba kiwango hicho hakitoshi.

Ufisadi ulivyozidisha madhila kwa maeneo hayo

Kwa ufupi majimbo 29 ndiyo yaliyoratibiwa na serikali kama maeneo yanayokumbwa na hali ngumu ya kimazingira.

Huduma muhimu mfano afya, maji, miundo msingi, na hata elimu bado ni changamoto na mara nyingi ukosefu wa huduma kama vile maji zimetajwa kuchochea uhasama miongoni mwa jamii hizo kama alivyosema Gavana wa Jimbo lenye ukame la Turkana, Josephat Nanok.

"Huduma za maji ni muhimu sana kwa maisha ya Jamii ya wafugajaii wa kuhamahama, pili ni Elimu na suala linguine linalopasa kuzingatiwa zaidi ni udumishwaji wa amani ili wakati maeneo haya yanapoimarika kiviwanda na uchumi kusiwepo ni migogoro ya kung'ang'ania rasilimali. Na mfano mzuri ni mzozo ulioshuhudiwa eneo la Turkana Mafuta yalipopatikana."

Naibu Rais William Ruto (kushoto), Gavana wa Turkana Josephat Nanok, Gavana wa Kilifi Amason Kingi wakati wa ufunguzi wa kwanza wa ASAL mjini Malindi, Kenya, Septemba 6, 2018.Picha: DW/E. Ponda

Maeneo haya yanasemekana kuwa na rasilimali zilizopo chini ya ardhi zinazoweza kubadilisha uchumi wa Taifa la Kenya, mfano mafuta ambayo hivi majuzi yamepatikana katika Jimbo  la Turkana.

 Balozi wa Marekani ambaye aliwakilisha taasisi na mashirika ya kigeni yanayojuhusisha zaidi na maendeleo ya sehemu hizi alisema kuwa Ufisadi umechangia pakubwa madhila yanayowakumba wakaazi wa sehemu hizi. "Ufisadi huwaogofya waekezaji wa kigeni na kuathiripakubwa ukuoaji wa uchumi. Na kwa namna hiyo pia kuathiri maendeleo ya uchumi wa  sehemu hizi  zenye ukame," alisema balozi  huyo Robert Godec .

Kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha umaskini visa vya utapiamlo vimekithiri katika sehemu hizi zenye ukame kukiwa na Watu million 3 na laki nne wanao kosa chakula mara kwa mara.

Mwandishi: Eric Ponda

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman


 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW