1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta amvaa naibu wake Ruto akimtaka ajiuzulu

Shisia Wasilwa
2 Mei 2022

Rais Uhuru Kenyatta amemtaka Naibu wake William Ruto kujiuzulu serikalini, miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu. Kenyatta ametoa kauli hiyo wakati alipohutubia taifa wakati wa sherehe za siku ya wafanyakazi Jumapili

Kenia Symbolbild Wahlen und Social Media
Picha: AFP/T. Karumba

Matamshi ya Rais yanajiri, huku uhusiano kati yake na naibu wake ukiendelea kusambaratika, ishara kuwa Kenyatta ameamua kwa vyovyote vile viwavyo kutomuachia Ruto kiti hicho. Rais Kenyatta alimtuhumu Ruto kwa kuwachochea wananchi baada ya bei za mafuta kuongezeka, huku baadhi ya wauzaji wakihodhi bidhaa hiyo muhimu.

Akijitetea Rais amesema changamoto za ongezeko la gharama ya maisha, zimetokana na vita vinavyoendelea nchini  Ukraine pamoja na athari za janga la Covid-19. Nyufa za  mahusiano kati ya Rais na naibu wake zilizioanza kudhihirika mwaka 2018, zilibainika wazi wakati wa mazishi ya Rais mstaafu Mwai Kibaki. Rais hakumsalimu naibu wake wakati wa kuutazama mwili wake marehemu.

"Badala ya kunisaidia kuona wananchi watasaidika vipi, yuko kule sokoni na matusi na unajiita kiongozi, si uondoke nitafute mwingine!”

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Katika mazishi ya Kibaki, Ruto alimtaja rais huyo wa zamani kuwa bora miongoni mwa marais ambao Kenya imewahi kuwa nao, matamshi ambayo huenda hayakuchukuliwa vizuri na bosi wake. Hata hivyo, Ruto ambaye alikosa kuhudhuria sherehe za Mei Mosi hakusita kumjibu Rais.Odinga awa rasmi mpizani wa Ruto

Kwenye mtandao wake wa twitter, Ruto aliandika kuwa, "Samahani bosi wangu. Nahisi maumivu yako. Wale uliowapa majukumu yangu pamoja na yule mzee, kwa maana ya Raila Odinga wamekufeli vibaya.

Walivuruga mpango wa ajenda nne kuu, wakaangamiza chama chetu na kukuharibia wakati. Bosi mimi napatikana. Nipigie tu simu.” Naye Seneta Moses Wetangula amemsuta rais kwa msimamo wake dhidi ya Ruto.

Hii ndio mara ya kwanza kwa rais na naibu wake kujibizana hadharani tangu wakosane bila ya kutumia vijembe. Rais Kenyatta ana miezi mitatu tu kuachia madaraka, hata hivyo ameonesha bila kuficha kuwa anamuunga mkono Raila Odinga. Aliahidi kumfanyia kampeini.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW