1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta aongeza tena vizuizi dhidi ya corona

27 Julai 2020

Rais Uhuru Kenyatta amekaza masharti ya kukabiliana na virusi vya corona nchini Kenya. Wananchi watazuiliwa kutoka majumbani kuanzia mwendo wa saa tatu usiku hadi saa kumi alfajiri kwa siku nyingine 30.

Kenia Coronavirus Uhuru Kenyatta
Picha: PSCU

Siku 21 baada ya rais Uhuru Kenyatta kulegeza masharti ya kukabiliana na janga la virusi vya korona, visa vya maambukizi hayo vinaonekana kuongezeka maradufu nchini Kenya. Akilihutubia taifa kwa mara ya kumi tangu janga la Corona lilipobisha nchini rais Kenyatta alielezea wasiwasi wake kuhusu kasi ya maambukizi ya virusi hivyo. Kati ya majimbo 47 majimbo 44 yameathiriwa na ugonjwa huo. Aidha watu 17603 wameambukizwa virusi hivyo kote nchini. Vilabu vya burudani vikitajwa kuwa vyenye hatari ya kusambaza maambukizi.

Kiwango kidogo cha maambukizi kimetajwa kuwa sababu inayowapa baadhi ya wakenya ya kuvunja masharti ya kukabiliana na maradhi ya Covid-19. Rais Kenyatta alisisitiza wito wake kuwa serikali haiwezi ikawalinda raia wote, kwani jukumu la kukabiliana na ugonjwa huo ni la kila mmoja. 

Mfanyakazi wa maabara Jeremie Omari akivaa mavazi ya kujikinga kabla ya kuanza kazi zake nchini Kenya.Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Inganga

Mikutano ya hadhara ya wanasiasa ingali imepigwa marufuku, huku serikali ikiwataka wote ambao watahudhuria mazishi kuzingatia masharti ya wizara ya Afya. Akitoa mifano ya mataifa ambayo yameathiriwa zaidi, rais Kenyatta alisema serikali yake haiwezi kukubali, Kenya kufuata mkondo huo.

Kenya imepoteza zaidi ya watu 200 tangu janga hilo lilipolipuka mapema mwezi wa tatu mwaka huu na huenda idadi hiyo ikaongezeka. Awali baraza la magavana lilikuwa linapendekeza Jiji la Nairobi kufungwa kwani ndilo chimbuko la maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19. Wycliffe Oparanya ni mwenyekiti wa baraza la magavana.

Vilabu vya burudani vitakavyopatikana vikikiuka masharti hayo, vitanyang'aywa leseni zao. Rais Kenyatta alilegeza masharti mwezi uliopita, baada ya wakenya wengi kulia kuwa maisha yao yalikuwa magumu. Inspketa Mkuu wa Polisi ametakiwa kuhakikisha kuwa sharia inazingatiwa kwa kila mkenya bila ya kujali hadhi ama cheo cha mtu. Asilimia 70 ya majimbo yamejiandaa kwa mlipuko mkubwa wa janga la Corona kwa mujibu wa serikali.

Shisia Wasilwa, DW, Nairobi