Kenyatta aongoza
5 Machi 2013Huku kiasi cha robo moja ya kura kikiwa kimeshahisabiwa, matokeo ya awali yanaonesha kuwa Kenyatta, ambaye pia ni naibu waziri mkuu, anaongoza kwa asilimia 54 ya kura, akifuatiwa na Waziri Mkuu Raila Odinga mwenye asilimia 41.
Hata hivyo, ni kura chache zilizokuwa zimehisabiwa kutoka kwenye ngome ya Odinga, mji wa Kisumu ulio magharibi mwa Kenya, na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imesema kwamba matokeo yatakamilika kufikia kesho Jumatano (tarehe 6 Machi).
Hapo jana Jumatatu (tarehe 4 Machi), wapiga kura walijitokeza kwa wingi kupiga kura. Maafisa wa IEBC wanakisia kwamba kiasi cha asilimia 70 ya raia milioni 14 waliojiandikisha, wamepiga kura zao.
Kwa upande mwengine, mashambulizi yanayoshukiwa kufanywa na makundi ya watu wanaotaka kujitenga kwenye eneo la pwani ya Kenya yaliua watu 19 hapo jana, huku mashambulizi mengine yakiripotiwa kwenye mpaka wa nchi hiyo na Somalia, ingawa sehemu kubwa ya nchi ilipiga kura kwa amani.
Hali ni shwari
Hadi asubuhi ya leo Jumanne (tarehe 5 Machi), mji mkuu Nairobi ulikuwa kimya na hakukuwa na matukio mengine ya ghasia yaliyoripotiwa kutoka maeneo mengine ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki, ambayo katika uchaguzi mkuu uliopita ilishuhudia maafa makubwa.
Kenyatta anakabiliwa na mashitaka kwenye mahakama ya ICC, ambako anatuhumiwa kusaidia katika uchochezi wa ghasia za baada ya uchaguzi hapo mwaka 2007-2008 ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuawa.
Marekani na mataifa mengine ya Ulaya yameonya juu ya "matokeo mabaya", ikiwemo mataifa hayo kulazimika kukata mawasiliano na Kenyatta atachaguliwa kuwa rais, kwa sababu ya kukabiliwa kwake na kesi hiyo mbele ya ICC.
Mara baada ya Rais Mwai Kibaki kutangazwa kuwa mshindi kwenye uchaguzi wa mwaka 2007, wafuasi wa Odinga waliingia barabarani, hatua ambayo ilianzisha miezi miwili ya mashambulizi ya kikabila. Mbali ya zaidi ya watu 1,000 kuuawa, wengine zaidi ya 600,000 walilazimishwa kuyahama makaazi yao.
Maafisa wa serikali wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha kwamba kiwango kama hicho cha ghasia hakirejelewi mara hii, huku wagombea wote wawili wakuu - Odinga na Kenyatta - wakiahidi kukubaliana na matokeo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Mohamed Abdulrahman