1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta: Operesheni imekamilika na magaidi wote wameuawa

Sylvia Mwehozi
16 Januari 2019

Operesheni katika hoteli ya Dusit jijini Nairobi imekamilika huku watu 14 wakithibitishwa kuaga dunia. Rais Uhuru Kenyatta amesema magaidi wote wameuawa huku zaidi ya watu 700 wakiokolewa.

Nairobi Angriff auf Hotel in Kenias Hauptstadt
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Inganga

Saa 24 baada ya operesheni ya kuwakabili magaidi kufanyika katika hoteli ya Dusit inayopakana na ubalozi wa Australia, imekamilika. Kwenye picha za camera ya CCTV, washukiwa wanne wa kigaidi walionekana wakiingia kwenye jengo la hoteli ya kifahari ya Dusit ambayo ina ofisi, hoteli pamoja na benki na kuanza kushambulia watu kwa kuwapiga risasi. Eneo hilo ambalo ni maarufu kwa raia wa kigeni kwa sasa limewekwa uzio huku polisi wakizuia umma kufika pale. Rais Uhuru Kenyatta amepongeza vikosi vya usalama kwa kuwakabili magaidi hao.

"Magaidi wote wameuawa. Kwa wakati huu, tumethibitisha kuwa watu 14 wasio na hatia waliangamia kwa mkono wa wauaji hawa na wengine wakijeruhiwa,” alisema rais Kenyatta.

Milio ya risasi ilikuwa inasikika Jumatano asubuhi, katika ghorofa ya saba ya hoteli hiyo ishara kuwa kulikuwa na makabiliano baina ya vyombo vya usalama na magaidi kwa siku ya pili. Kwa mujibu wa maofisa kulikuwa na magaidi watano waliouawa na vyombo vya usalama huku mmoja akijitoa mhanga.  ni waziri wa usalama wa taifa.

Mama mmoja akiokolewa na mfanyakazi wa msalaba mwekunduPicha: Getty Images/AFP/L. Tato

"Jengo lote ambalo lilivamiwa sasa ni salama, vyombo vya usalama vimewaokoa idadi kubwa ya wakenya na raia wengine wa kigeni. Tuko kwenye harakati za kukamilisha shughuli hizi,” alisema Fred Matiangi waziri wa usalama wa taifa. 

Kwa sasa vyombo vya usalama vinaendelea kupekua jengo hilo na kutafuta ushahidi. Rais Uhuru Kenyatta amesema serikali yake itaendelea kuboresha usalama katika siku zijazo dhidi ya magaidi.

"Tumechukua tahadhari na tuko chonjo, nawahakikishia Wakenya na Wageni ya kwamba mko salama nchini Kenya,” alisema Kenyatta.

Duru zinasema kuwa raia wa Uingereza na Mmarekani ni miongoni mwa watu waliouawa. Wakati huo huo, Marekani na Umoja wa Mataifa zimelaani kitendo hicho. Msemaji wa idara ya Ulinzi wa Marekani amekitaja kitendo hicho cha uvamizi kuwa cha kipumbavu huku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akikitaja kuwa uvamizi mbaya wa kigaidi.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Nairobi

Mhariri: Josephat Charo 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW