1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta: Serikali chapeni kazi msilaumu utawala uliopita

Shisia Wasilwa
20 Novemba 2023

Rais Mstaafu wa kenya Uhuru Kenyatta, ameiambia serikali iliyoko madarakani iache kuulaumu utawala wake kwa kushindwa kutimiza malengo iliyowaahidi Wakenya.

Rais Mstaafu wa kenya Uhuru Kenyatta
Rais Mstaafu wa kenya Uhuru KenyattaPicha: Metin Aktas/Anadolu Agency/picture alliance

Uhuru amesema  serikali ya rais William Ruto  inapaswa kushughulikia matatizo yanayowakabili Wakenya badala ya kutafuta sababu zisizo na msingi. Shisia Wasilwa na ripoti kamili.

Matamshi ya Kenyatta yanajiri huku serikali ya Rais Ruto ikishindwa kudhibiti hali ya uchumi wa taifa ambayo imesababisha gharama ya maisha kupanda miaka miwili baada ya kupewa ridhaa na wakenya kuongoza taifa hilo lenye uchumi mkubwa Afrika ya Mashariki na Kati.

Rais Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua wamehusisha utawala wa Uhuru na gharama kubwa ya maisha ya sasa.

Soma pia:Wakenya walia na bei mpya za petroli na dizeli

Uhuru aliyasema hayo kwenye ibada ya Jumapili katika eneo la Mwingi kaunti ya Kitui alipokuwa amealikwa na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka.

Alisema kila mara mtu anaposhindwa kufanya anachopaswa kufanya, wanalaumu serikali iliyopita.

"Huu mwenendo hata kama mke amekataa kujifungua, tutalaumiwa sisi, lakini tumezoea hili,"

Shutuma za serikali dhidi ya utawala wa Uhuru

Mapema mwezi huu, Waziri wa Fedha Profesa Njuguna Ndung'u aliilaumu serikali iliyopita kuwa chanzo cha gharama kubwa ya maisha kwa madai ya kile alichokiita, makosa ya kiuchumi yaliyofanywa na serikali ya Rais aliyestaafu Uhuru Kenyatta.

Kama haitoshi, Wiki iliyopita, Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen nae pia  aliilaumu serikali iliyopita kwamba ndiyo iliyohusika na ujenzi wa paa la kuvuja katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Alipokuwa akifanya kampeini Ruto aliahidi kupunguza gharama ya maisha, suala ambalo laelekea kumpiga chenga sasa.

Maoni na matarajio ya Wakenya kwa utawala wa William Ruto

01:44

This browser does not support the video element.

Aidha Uhuru alisisitiza kuwa bado ni mwanachama wa muungano wa Azimio La Umoja na hana wasiwasi na mchezo wa kulaumiana unaondelea.

Soma pia:Serikali ya Kenya kudhibiti mfumuko wa bei

Alikuwa ameandamana na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Naibu kiongozi wa chama cha ODM Wycliffe Oparanya, kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, Gavana Wavinya Ndeti na naibu wake Francis Mwangangi na idadi ya wabunge wa Azimio.

Kalonzo aliishutumu serikali ya Ruto kuhusu kuongezeka kwa gharama ya maisha.

Rais mstaafu Uhuru alionekana mara ya mwisho hadharaniJulai 2023, boma la mwanawe wa kwanza, Jomo, lilipovamiwa na maafisa wa polisi kwa madai ya kumiliki bunduki kinyume cha sheria.

Rais mstaafu huyo, hata hivyo, alipofika kwa mwanawe, askari waliotumwa walitoroka, Uhuru akitaja kitendo hicho kama cha uwoga.

Alilaumu serikali ya Rais William Ruto, kwa kile alidai ni njama ya kuhangaisha familia yake.

Oktoba 26, Rais huyo wa tano wa Jamhuri ya Kenya aliadhimisha miaka 62 ya kuzaliwa japo hakuwa nchini.

Wanasiasa na Marafiki zake wa karibu waliandaa hafla ya kusherehekea kuzaliwa kwake.