1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry aikosoa Israel kuhusu sera yake ya ulowezi

29 Desemba 2016

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameikosoa Israel kwa kuendelea na mpango wake wa ujenzi wa makaazi ya walowezi, na kumtuhumu waziri mkuu Benjamin Netanyahu kuiburuza nchi hiyo kutoka kwenye demokrasia.

USA Außenminister John Kerry zu Lage in Nahost
Picha: Getty Images/Z. Gibson

Katika hotuba yake ya kuaga, Kerry alibainisha mkakati wa suluhisho la mataifa mawili ambao hatokuwepo madarakani kuutekeleza, lakini ambao Marekani ilitumai unaweza kuuheshimiwa hata baada ya kumalizika kwa muhula wa rais Barack Obama.

Alitetea hatua ya Obama wiki iliyopita kuliruhusu baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuyatangaza makaazi ya walowezi wa Kiyahudi kuwa haramu, katika hatua iliyosababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kidiplomasia kati ya Marekani na mshirika wake wa karibu zaidi katika kanda ya Mashariki ya Kati.

"Tusingeweza katika nia njema, kuzuwia azimio katika Umoja wa Mataifa linalobainisha wazi kuwa pande zote zinapaswa kuchukuwa hatua kulinda uwezekano wa amani," alisema Kerry katika hotuba hiyo iliodumu kwa zaidi ya saa moja mjini Washington.

"Ujerumani iko tayari kuchangia amani"

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameisifu hotuba ya Kerry na kuitaja kama onyo kwamba suluhisho na mataifa mawili halipaswi kuachwa kusambaratika na pia kama maagizo kwa pande mbili kuchukuwa hatua stahiki kuhakikisha suluhisho hilo linafikiwa, na kuongeza kuwa Ujerumani iko tayari kwa pamoja na washirika wake ndani ya Umoja wa Ulaya, kutoa mchango wao kwa amani ya Masahriki ya kati.

Waziri Kerry akiwa na Netanyahu katika mmoja ya mikutano yao mjini Jerusalem Desemba 13, 2013.Picha: Reuters

Netanyahu alijibu hotuba ya Waziri Kerry katika taarifa ilioandaliwa haraka kupitia televisheni, ambamo alisema amemalizana na utawala wa Obama na yuko tayari kufanya kazi na rais mteule Donald Trump, ambaye ameiunga mkono Israel kikamilifu. Kiongozi huyo wa Israel alimkosoa Kerry kwa kushikwa na makaazi ya walowezi akipuuza mashambulizi ya Wapalestina na uchochezi wa vurugu.

"Waziri Kerry amepuuza kampeni ya mfululizo ya ugaidi ilioendeshwa na Wapalestina dhidi ya taifa ya Kiyahudi kwa karibu karne nzima. Alichokifanya ni kutumia muda mwingi wa hotuba yake kuilaumu Israel kwa kukosekana kwa amani, kwa kulaumu kwa hisia sera ya kuwawezesha Wayahudi kuishi katika ardhi yao ya kihistoria na katika mji mkuu wao wa milele Juerusalem."

Mwisho mchungu kati ya Obama na Netanyahu

Lawama hizo za pande mbili zimeashiria kiwango cha chini kabisa katika uhusiano wa Marekani na Israel, na mwisho mchungu wa miaka minane ya uhusiano wa mivutano kati ya Obama na Netanyahu, ambao wamegombana mara kwa mara juu ya makaazi ya walowezi, mchakato wa amani na makubaliano ya Obama kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Trump, ambaye aliihakikishia Israel kwamba inahitaji kuvumilia hadi atakapochukuwa madaraka, hakusema Jumatano iwapo ujenzi wa makaazi ya walowezi unapaswa kuzuwiwa. Lakini aliwaambia waandishi habari kuwa Israel ilikuwa inatendewa isivyo haki na watu wengi tofauti.

Na haikubanika iwapo suala la Israel lilizungumziwa katika mazungumzo ya simu ambayo Obama alimpigia Trump wakati akiwa mapumzikoni mjini Hawaii Jumatano asubuhi. Na wala haikuwa bayana nini itakuwa athari ya hotuba ya Kerry, ambayo imekuja katika siku za mwisho wa utawala wa Obama.

John Kerry akiwa na Mahmoud Abbas mjini Ramallah 05.12.2013 katika juhudi zake za kuleta amani baina ya Wapalestina na Waisrael.Picha: Reuters/Mohamad Torokman

Abbas: Tuko tayari kuzungumza tena ikiwa...

Marekani, Wapalestina na sehemu kubwa ya ulimwengu wanapinga ujenzi wa makaazi ya walowezi katika eneo la ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, ambayo ni maeneo yalioporwa na Israel mwaka 1967 na yanayodaiwa na Wapalestina kwa taifa lao huru.

Kerry alisema suluhisho la mataifa mawili, ambalo ndiyo msingi wa mazungumzo ya amani kwa miaka yote, lilikuwa katika hatari kubwa, na kuitaja serikali ya Netanyahu kuwa yenye msimamo mkali zaidi wa mrengo wa kulia katika historia ya taifa hilo.

Kwa upande wake rais wa mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas alijibu hotuba ya Kerry kwa kusisistiza utayarifu wake kurejea mazungumzo ikiwa Israel itasitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/Ape,rtre,afpe

Mhariri: Daniel Gakuba