1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry aitaka dunia kuchukua hatua zaidi kwa Syria

19 Julai 2013

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kuuangalia mzozo wa kibinadamu nchini Syria kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

US Secretary of State John Kerry speaks during a joint press conference as Jordan's Foreign Minister Nasser Judehlooks on, on July 17, 2013 at the Ministry of Foreign Affairs in Amman. Kerry met with Arab League officials to discuss his push to thaw out the frozen peace process, as Palestinians said there had been progress. AFP PHOTO/Mandel NGAN-POOL (Photo credit should read MANDEL NGAN/AFP/Getty Images)
John Kerry akiwa mjini Amman pamoja na waziri mwenzake wa Jordan Nasser JudehPicha: Mandel Ngan/AFP/Getty Images

Kerry ameyasema hayo baada ya kutembelea kambi ya wakimbizi wa Syria nchini Jordan. Wakati huo huo benki kuu ya dunia imeidhinisha mkopo wa dola milioni 150 kwa Jordan kuisaidia nchi hiyo kupambana na gharama za kuwahudumia maelfu ya wakimbizi wa Syria ambao wamekimbilia nchini humo.

Baada ya Kerry kukutana na wakimbizi wa Syria katika kambi ya Zartari , amesema kuwa "nafikiri wamefadhaika na wameikasirikia dunia kwa kutochukua hatua za kuwasaidia.

Kamishna wa UNHCR Antonio GuterresPicha: Reuters

Katika sehemu ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu katika eneo la mashariki ya kati , Kerry ameitembelea kambi hiyo kaskazini mwa Jordan, kambi ambayo ina ikiwa na wakimbizi 160,000 raia wa Syria imewekwa kuwa ni kambi ya pili kubwa kabisa ya wakimbizi duniani.

Wakimbizi waandamana

Mara Kerry alipowasili , kiasi ya wakaazi 200 wa kambi hiyo walifanya maandamano wakiitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kati nchini Syria.

"Liko wapi eneo ambalo haliruhusiwi ndege kuruka?" waliimba watu hao, kwa mujibu wa watu walioshuhudia.

"Ziko wapi silaha kwa wanamapinduzi? Tunakufa huku mkiwa kimya." Wamesema watu hao.

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR , Antonio Guterres ametoa wito kama huo wa John Kerry wakati alipoutaka Umoja wa Ulaya kuwachukua wakimbizi zaidi wa Syria badala ya kutegemea nchi jirani na Syria kubeba mzigo huo mkubwa.

Umoja wa Ulaya haujachukua hatua

"Umoja wa Ulaya katika siku za nyuma uliitaka Uturuki kuweka mipaka yake wazi kwa wakimbizi kutoka Syria ambao wanataka kuomba hifadhi , wakati huo huo umoja huo ukielekeza nguvu zake katika kujaribu kudhibiti watu wanaoingia kinyume na sheria katika mipaka yake , " mkurugenzi huyo wa shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa amewaambia mawaziri wa sheria wa umoja huo katika mkutano wao mjini Vilnius.

Wakimbizi wa Syria nchini JordanPicha: picture-alliance/dpa

Marekani ni moja kati ya wafadhili wakubwa wa Jordan , ambayo imefungua milango yake kwa zaidi ya Wasyria 560,000 tangu yalipozuka mapigano ya wenyewe kwa wenyewe Machi 2011. Marekani pia imetoa dola milioni 54 kwa ajili ya msaada wa dharura wa kiutu mwezi uliopita.

Jana Alhamis(18.07.2013) , bodi ya magavana wa benki kuu ya dunia imeidhinisha dola milioni 150 za msaada wa dharura kwa Jordan kuisaidia nchi hiyo kupambana na wimbi la wakimbizi wanaoingia nchini humo , kwa kuisaidia sekta ya afya ya nchi hiyo na kutoa msaada kwa raia wa Jordan wanaokabiliwa na kupanda kwa bei za vyakula.

Familia ya wakimbizi wa SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Vita nchini Syria imesababisha watu milioni 6.5 kukimbia makaazi yao , ikiwa ni pamoja na watu milioni 4.2 ambao wamekimbia makaazi yao ndani ya Syria. Kiasi ya watu 93,000 wameuwawa katika vita hivyo tangu karibu miaka mitatu iliyopita.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / ape

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi