1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry akutana na Rais Xi wa China

14 Februari 2014

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amekutana na Rais Xi Jinping wa China Ijumaa(14.02.2014)wakati kukiwa na mvutano wa maeneo ya bahari kati ya washirika wake Japani na Ufilipino dhidi ya madai ya China.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akikutana na Rais Xi Jinping wa China mjini Beijing. (14.02.2014).
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akikutana na Rais Xi Jinping wa China mjini Beijing. (14.02.2014).Picha: Reuters

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry ameomba msaada wa China katika kuirudisha Korea Kaskazini katika mazungumzo ya kutokomeza silaha za nuklea lakini ombi hilo linaweza lisiitikiwe vyema kutokana na kuambatana na madai ya kuitaka serikali ya China ipunguze hatua zake za uchokozi inazochukuwa kuweka mabavu yake katika mzozo wa mipaka ya bahari na nchi ndogo jirani zake.

Kerry ameanza ziara yake hiyo ya saa 24 kwa kukutana na Rais Xi Jinping wa China katika Ukumbi Mkuu wa Wananchi mjini Beijing na baadae alikuwa anatazamiwa kukutana na maafisa mbali mbali waandamizi wa serikali ya China kuelezea azma ya utawala wa Rais Barack Obama wa kuupa uzito mpya sera yake ya kigeni kwa eneo la Asia na Pasifiki wakati kukiwa na matatizo mengine lukuki ya dunia yanayohitaji kupewa kipau mbele.Kerry anatazamiwa kuzungumzia na wenyeji wake masuala kuanzia ya mabadiliko ya tabia nchi hadi Syria na Iran.

Hata hivyo anakabiliwa na kibaruwa kigumu kunadi hoja zake katika agenda zake kuu mbili: Korea Kaskazini na kuibuka kwa mvutano wa mipaka ya bahari katika kanda hiyo hususan kutokana na madai ya Japani ya kuwania mipaka hiyo ya bahari na China.

China ilipuuza kwa ghadhabu shutuma za Marekani kutokana na hatua zake ilizochukuwa katika bahari ya Mashariki na China Kusini ambazo zimewatia wasi wasi washirika wa Marekani Japani na Ufilipino.

Shinikizo liwe kwa Japani

Katika uhariri dhidi ya Japani shirika la habari la serikali nchini China Xinhua limesema leo hii Marekani inapaswa kushinikiza Japani kuachana na hatua zake za uchokozi venginevyo iwe tayari kukabiliana na hatari ya kuzusha mzozo wa kanda katika kipindi cha usoni.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akiwa pamoja na waziri mwenzake wa China Wang Yi mjini Beijing.(14.02.2014).Picha: picture-alliance/AP

Shirika hilo limesema Marekani inabidi ijuwe kwamba wakati China daima imekuwa ikijaribu kutatuwa matatizo ya mipaka ya bahari na baadhi ya nchi jirani kwa njia za amani,haitosita kuchukuwa kuhakikisha maslahi yake makuu ya usalama wa taifa kwa haki ya kutawala ardhi yake.

Xinhua imesema kile inachotakiwa kufanya Marekani hivi sasa sio kuilaumu China bali kuishinikiza Japani kuachana na vitendo vyake vya uchokozi.

Kutokomeza silaha za nuklea

Akiwa katika mji mkuu wa Korea Kusini Seoul hapo jana waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema utawala wa Obama unataka kuweka mkazo mpya katika kirudisha Korea Kaskazini katika mazungumzo ya pande sita yaliokwama yenye lengo la kuifanya Korea Kaskazini iachane na silaha za nuklea.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akiwasili Seoul,Korea Kusini. (13.02.2014).Picha: Chung Sung-Jun/Getty Images

Kerry amewaambia waandishi wa habari anataka ifahamike wazi Marekani haitokubali Korea Kaskazini liwe taifa lenye kumiliki silaha za nuklea na hawatokubali kufanya mzungumzo kwa minajili tu ya kuwa na mazungumzo. Ameitaka Korea Kaskazini ionyeshe kwamba iko tayari kuzungumza na kutimiza ahadi zake za kuondokana na silaha za nuklea.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW