1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry ataka mzozo wa Kongo umalizwe

26 Julai 2013

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry ameutaka Umoja wa Mataifa kusaidia kumaliza mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, baada ya kuwepo taarifa waasi wa eneo hilo wanapata msaada kutoka nje.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John KerryPicha: Reuters

Hata hivyo, Kerry hakuitaja nchi yoyote kuhusika na tuhuma hizo ingawa ujumbe huo ulilengwa kwa Rwanda.

Akizungumza mjini New York katika Umoja wa Mataifa, Kerry, ameliambia baraza la usalama la umoja huo kwamba Marekani ina wasiwasi sana kuhusu taarifa za msaada mpya unaotolewa na watu wa nje kwa kundi la waasi la M23 linalopambana na vikosi vya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Kerry alisisitiza na kuwataka wale wote wanaowasaidia waasi wa M23 kuacha kufanya hivyo na kwamba serikali zote lazima ziwakamate watu wanaokikua haki za binaadamu.

Rwanda yahusishwa

Ingawa Kerry hakuitaja nchi yoyote, Jumanne iliyopita, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Jen Psaki, alisema Marekani inaamini kuna ushahidi wa kutosha kusaidia utafiti uliofanywa na Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, ikiwemo tuhuma kwamba Rwanda inawasaidia waasi wa M23 na ushahidi unaowaunganisha maafisa wa juu wa jeshi la Rwanda na waasi.

Waasi wa Kongo wa M23Picha: Phil Moore/AFP/Getty Images

Psaki alisema wanaitaka Rwanda kuacha mara moja kulisaidia kundi la M23 na kuwaondoa wanajeshi wake mashariki mwa Kongo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana kudurusu ulipofikia mpango wa kuanza kuutekeleza mkataba wa amani uliosainiwa Februari 24 na mataifa 11 ya Afrika ili kumaliza mzozo wa mashariki mwa Kongo.

Rwanda ambayo ina kiti katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa miaka miwili, pia imekubali wito wa kuzitaka nchi zote kuacha kujihusisha na masuala ya Kongo na kuunga mkono mpango huo wa amani unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Rwanda ambayo ni miongoni mwa nchi 11 zilizosaini mkataba huo wa amani, imekanusha madai ya kuhusika kwa namna yoyote kuwasaidia waasi wa M23.

Umoja wa Mataifa walizungumzia pia kundi la FDLR

Ama kwa upande mwingine, taarifa ya baraza hilo imeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa shughuli za kundi la Wahutu lenye silaha la FDLR mashariki mwa Kongo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo, Raymond Tshibanda, amekanusha vikali kuwa nchi yake inawaunga mkono FDLR na kuahidi kuwa haki itatendeka kutokana na wale wanaohusika na vitendo vya ubakaji na unyanyasaji.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo, Raymond TshibandaPicha: picture-alliance/dpa

FDLR, linashutumiwa kuhusika na mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 na imeripotiwa kuwa linafanya mashambulizi katika ardhi ya Rwanda.

Katika mkutano huo wa Umoja wa Mataifa, suala la mzozo wa Syria pia liligusiwa, ambapo kiongozi wa kundi la upinzani nchini Syria linaloungwa mkono na nchi za Magharibi aliitaka Marekani kupeleka haraka msaada wa kijeshi ilioahidi ili kuzuia ushindi wa jeshi la Rais Bashar al-Assad.

Ahmad Al-Jarba, kiongozi wa Muungano wa Kitaifa wa Syria, amesema hali nchini Syria ni ya kukatisha tamaa na upinzani unahitaji kwa dharura hatua ya Marekani kuwapa silaha waasi haraka na kuendelea kuishinikiza jumuiya ya kimataifa ili suluhisho la kisiasa liweze kupatikana.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,AFPE
Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi