1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry azuru jimbo la Wakurdi wa Iraq

24 Juni 2014

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amezuru jimbo lenye mamlaka yake ya ndani la Wakurdi nchini Iraq katika harakati za kidiplomasia kushinikiza kusikilizana kwa makundi ya nchi hiyo ili kuizuwiya isigawanyike.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry (kushoto) na Rais Massud Barzani wa Mamlaka ya Ndani ya Wakurdi (kulia) mjini Arbil Iraq. (24.06.2014)
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry (kushoto) na Rais Massud Barzani wa Mamlaka ya Ndani ya Wakurdi (kulia) mjini Arbil Iraq. (24.06.2014)Picha: Reuters

Rais wa mamlaka ya ndani ya Kurdsitan Massud Barzani amemuambia Kerry kwamba kutokana na mabadiliko yanayotokea nchini humo wanakabiliwa na uhalisia mpya na Iraq mpya akikusudia mashambulizi ya wanamgambo wa Kisunni ambayo yamezikumba sehemu za kaskazini na magharibi ya Iraq.

Kerry amewasili Arbil Jumanne ( 24.06.2014) baada ya hapo jana kuwa na mazungumzo mjini Baghdad na viongozi wa Kisunni na Waziri Mkuu Nuri al- Maliki.

Akimkaribisha Kerry katika kasri lake la rais,Barzani amemwambia mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu kabisa wa Marekani kupitia mkalimani kwamba Wakurdi wanatafuta ufumbuzi wa mzozo huo walioushuhudia.

Wakurdi nao wateka maeneo

Mashambulizi ya wanamgambo wa Kisunni yamewawezesha pia Wakurdi wa Iraq ambao waliwahi kunyunyuziwa gesi ya sumu na dikteta Saddam Hussein kuchukuwa udhibiti wa maeneo makubwa ya ardhi yenye mzozo ambayo walikuwa wakidai kuyajumuisha kwenye mamlaka ya jimbo lao,madai ambayo yalikuwa yakipingwa vikali na serikali ya Iraq.

Vikosi vya Wakurdi katika mji wa Kirkuk.Picha: Reuters

Vikosi vyao vya usalama hivi sasa vinawajibika na usalama wa mji wenye utajiri wa mafuta wa Kirkuk wenye mchanganyiko wa makabila ambao ni kitovu cha mzozo wa ardhi nchini humo.

Katika mazungumzo hayo na Rais Barzani wa Mamlaka ya jimbo la Kurdistan Kerry amekaririwa akisema "Changamoto ya kuunda serikali ni changamoto kuu ambayo tunakabiliana nayo.Ushirikiano wa usalama wa siku za hivi karibuni kati ya vikosi vilioko katika eneo hili la Wakurdi ni muhimu sana katika kuwadhibiti wanamgambo wa kundi la ISIL."

Marekani ina shauku ya kuyashawishi makundi ya Iraq kuharakisha uundaji wa serikali mpya kufuatia uchaguzi wa mwezi wa Aprili.

Maliki chanzo cha vurugu

Kabla ya mazungumzo hayo ya leo Barzani alikiambia kituo cha televisheni cha CNN cha Marekani kwamba Maliki anapaswa kujiuzulu kwa kuwa anahusika na kile kilichotokea.

Rais Masud Barzani wa Mamlaka ya Ndani ya jimbo la Kurdistan nchini Iraq.Picha: Safin Hamed/AFP/Getty Images

Amesema katika kipindi cha miaka 10 iliopita wamefanya kila wawezalo kuijenga Iraq mpya yenye demokrasia lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kufanikiwa.

Alipoulizwa iwapo Wakurdi wa Iraq watagombania kupatiwa uhuru wao Barzani amekiambia kituo hicho kwamba wakati umefika kwa wananchi wa Kurdistan kuamuwa juu ya mustakbali wao na uamuzi wa wananchi ndio utakaoheshimiwa.

Chini ya mfumo wa utawala uliopo hivi sasa nchini Iraq, Wakurdi kwa desturi ndio wanaoshikilia wadhifa wa urais, Waarabu wa madhehebu ya Shia hushikilia wadhifa wa waziri mkuu na Waarabu wa madhehebu ya Sunni wanashikilia wadhifa wa spika wa bunge.

Marekani inaona Wakurdi wana dhima muhimu ya kutimiza katika kudumisha utengamano nchini humo.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman