1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry azuru makumbusho ya Hiroshima

11 Aprili 2016

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry amefanya ziara ya kihistoria kwenye makumbusho ya wahanga wa bomu la atomiki lililorushwa kwenye mji wa Japan, Hiroshima, wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Picha: Getty Images/AFP/K. Nogi

Kerry ambaye aliongozana na mawaziri wenzake wa mambo ya nchi za nje wa kundi la mataifa saba tajiri duniani-G7, za Uingereza, Ufaransa, Canada, Ujerumani, Italia na Japan kuzuru makumbusho hayo, anakuwa mwanadiplomasia mwandamizi wa kwanza wa Marekani kuzuru eneo hilo na ameelezea jinsi alivyoguswa katika ziara hiyo ya Hiroshima.

''Nataka kuelezea binafsi jinsi nilivyoguswa sana na heshima niliyopata kuwa waziri wa kwanza wa mambo ya nje wa Marekani kuzuru mji huu mzuri wa Hiroshima. Mapema leo kama mnavyojua, niliungana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Fumio Kishida pamoja na mawaziri wengine katika ziara yetu kwenye makumbusho haya ya ajabu ya amani,'' alisema Kerry.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuweka shada la maua kwenye makumbusho hayo, Kerry amesema kila mmoja anatakiwa kuzuru mji wa Hiroshima, ambako zaidi ya Wajapan 140,000 waliuawa kwa bomu la atomiki ambalo lilidondoshwa na Marekani Agosti 6, 1945.

Mawaziri wa G7 wakiwa HiroshimaPicha: Reuters/J. Ernst

Ziara hiyo inaonekana kama inaongeza matarajio huenda Rais wa Marekani, Barack Obama akazuru eneo hilo mwezi ujao, wakati atakapohudhuria mkutano wa kilele wa mwaka wa viongozi wa mataifa yanayounda kundi la G7, nchini Japan.

Ziara imefanyika pembezoni mwa mkutano wa mawaziri wa G7

Ziara hiyo imefanyika baada ya mawaziri hao wa mambo ya nje wa kundi la G7 kumaliza mkutano wao wa siku mbili ambapo kwa pamoja wamekubaliana kushinikiza kuwepo na dunia isiyotumia silaha za nyuklia. Wanadiplomasia hao waandamizi wa kundi la G7 wamesema katika azimio lao la pamoja kwamba wanathibitisha dhamira yao ya kuwepo na dunia salama kwa wote na kwa kujenga mazingira ya dunia isiyokuwa na silaha za nyuklia, ambazo kwa njia moja ama nyingine husababisha kukosekana kwa utulivu wa kimataifa.

Kerry amesema ana matumaini ziara hiyo inaonyesha umuhimu wa kukuza amani na kuimarisha uhusiano wa washirika imara ambao wameujenga pamoja kwa ajili ya kuwa na dunia iliyo salama na kushirikiana kuhakikisha dunia haina silaha za maangamizi.

John Kerry (kushoto), Fumio Kishida (kati) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Philip HammondPicha: Getty Images/AFP/J. Ernst

Kauli hiyo inaonyesha makubaliano yaliyofikiwa kwenye mazungumzo ya mawaziri hao na kuhusu majaribio ya ufyatuaji wa makombora yaliyofanywa hivi karibuni na Korea Kaskazini, ambapo wamesema hivyo ni vitendo vya kiuchokozi. Siku ya Jumamosi, Korea Kaskazini ilisema imefanikiwa kufanya jaribio la kombora lake ambalo linaweza kuishambulia Marekani.

Kerry amesema leo kuwa Marekani imejiandaa kuongeza shinikizo kwa Korea Kaskazini baada ya vitendo vyake vya uchokozi vya hivi karibuni, lakini bado imeacha milango wazi kwa ajili ya mazungumzo. Amesema bado kuna uwezekano wa kuongeza shinikizo zaidi, kulingana na vitendo vya Korea Kaskazini, lakini wameweka wazi kwamba wamejiandaa kwa mazungumzo ya amani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP,AFP,RTR,DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi