Kerry kujiunga na mazungumzo kuhusu Iran
23 Novemba 2013Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani zinaonekana kuwa katika ukingo wa kupata mafanikio katika mkwamo uliokuwapo kwa muongo mmoja sasa katika mzozo huo.
Mawaziri wa mambo ya kigeni wa China, Ufaransa , Uingereza na Ujerumani , Wang Yi, Laurent Fabius, William Hague na Guido westerwelle, wanatarajiwa kushiriki katika majadiliano makali kuhusiana na makubaliano ambayo Iran itazuwia shughuli zake za kinuklia ili kuweza kupata unafuu wa vikwazo vya kiuchumi.
Tangazo hilo limekuja baada ya wanadiplomasia katika mji huo wa Uswisi kusema kuwa masuala muhimu katika mazungumzo hayo, ambayo yalianza siku ya Jumatano huenda yametatuliwa.
Maafikiano yakaribia
Mwanadiplomasia mwandamizi kutoka bara la Ulaya amewaambia waandishi habari mapema kuwa mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa sita watakuja mjini Geneva iwapo tu kutakuwa na makubaliano ya kutiwa saini. "tumepiga hatua, ikiwa ni pamoja na masuala ya msingi," amesema mwanadiplomasia huyo.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amewasili mjini Geneva siku ya Ijumaa jioni na amekutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif na mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton, amesema msemaji wa Urusi.
Kerry anakwenda mjini Geneva " akiwa na lengo la kuendeleza hatua ya kupunguza tofauti na kusogea karibu na makubaliano," msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Jen Psaki amesema. Uamuzi ulichukuliwa baada ya kushauriana na Ashton , ambaye ni mratibu wa mazungumzo hayo na Iran kwa niaba ya mataifa ya Marekani , Urusi , China , Ufaransa, Uingereza na Ujerumani, amesema Psaki.
Mkwamo huenda umemalizika
Baadaye naibu msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Marie Harf amesema kuwa Kerry ameamua kwenda mjini Geneva "kutokana na hatua za maendeleo zilizofikiwa" na akiwa na "matumaini kwamba makubaliano yatafikiwa".
Likielezea matumaini kwamba makubalino yako karibu, shirika la habari la China Xinhua limemnukuu msemaji wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo akisema kuwa mazungumzo hayo " yamefikia hatua za mwisho". Waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo ameondoka mjini Beijing kwenda Geneva mapema leo Jumamosi (23.11.2013).
Wanadiplomasia wamesema kuwa maridhiano kuhusiana na msisitizo wa Iran kwamba "haki yake" ya kurutubisha madini ya urani itambulike kimataifa imependekezwa, huenda ikafungua njia ya kupatikana kwa maendeleo katika mkwamo uliopo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Bruce Amani