Kerry kutangaza mkakati wa amani Mashariki ya Kati
28 Desemba 2016Lengo la kupatikana kwa suluhisho la mataifa mawili ambapo Israel na taifa la baadae la Palestina yanaishi sambamba kwa kuzingatia mipaka iliyokubaliwa limevikwepa vizazi kadhaa vya wanadiplomasia wa Marekani.
Lakini katika siku za mwisho za utawala wa rais Barack Obama, na wakati ambapo serikali ya Israel ikionesha uhasama wa wazi kwa shinikizo la nje, Kerry anataka kuacha alama yake.
Hotuba yake hiyo inatarajiwa kuwa neno la mwisho la utawala wa Obama kuhusu mgogoro huo wa miongo kadhaa ambao Kerry alikuwa na matumaini ya kuutatua wakati wa muhula wake wa miaka minne kama mwanadiplomasia wa juu kabisaa wa Marekani.
Changamoto zinazomkabili
Nchini Israel inaweza kuonekana kama shinikizo la mwisho kwa waziri mkuu Benjami Netanyahu, ambaye amakuwa hasa na uhusiano mchungu na rais Obama tangu wawili hao walipoingia madarakani mwaka 2009.
Majadiliano kati ya Netanyahu na rais wa mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas tayari yamekwama, na ikiwa Kerry anataka pande hizo mbili kutilia maanani mpango wake mpana wa utatuzi, anakabiliwa na changamoto kuu mbili ambazo hata watangulizi wake walioshindwa hawakukumbana nazo.
Kwanza kabisaa ni hasira za Netanyahu dhidi ya utawa wa Obama kwa kushindwa kuzuwia azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lililolaani ujezi wa makaazi ya walowezi. Na pili rais ajae Donald Trump ameashiria atachukuwa msimamo laini, akimteuwa balozi ambaye anataka kuuhamishia ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem.
Abbas aeleza matumaini ya uhuru 2017
Viongozi wa Kiarabu wanaonya hatua kama hiyo itasababisha upinzani wa kikanda na maandamano ya Wapalestina, na Netanyahu hana motisha ya kuchukuwa hatua kabla ya Trump kukabidhiwa madaraka. Lakini rais Abbas ameelezea matumaini kuwa mkutano wa kimataifa utasaidia kuweka ratiba ya uhuru wa nchi yake na kukomesha ujenzi wa makaazi ya walowezi.
"Tunadhani na tunaamini kuwa azimio la Umoja wa Mataifa linaweka msingi wa wazi kwa Israel na dunia nzima kwamba wanapaswa kuanzisha majadiliano kwa msingi wa azimio hilo na kutoukataa uhalali wa kimataifa uliotamkwa bayana katika azimio hilo. Nawapongeza kwa azimio hilo na natumaini hatua zaidi zitafuata ili kukomesha ukaliaji wa aIsrael katika mwaka wa 2017," alisema wakati wa mkutano wa chama chake cha Fatah siku ya Jumanne.
Katika hotuba hiyo itakayotolewa mjini Washington, waziri Kerry atazungumzia hatua ya Marekani kujizuwia kwenye kura juu ya azimio la Umoja wa Mataifa ambalo lilipita kwa kura 14 bila hata moja ya kulikataa. Hotuba yake pia itazungumzia kile maafisa walichokitaja kuwa tuhuma za upotoshaji za maafisa wa israel kwamba utawala wa Obama uliandaa na kulaazimisha kupitishwa kwa azimio hilo.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre.
Mhariri: Lilian Mtono