1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry kuuzungumzia mzozo wa Mali

22 Februari 2013

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry mwishoni mwa juma hili anatarajiwa kuanza ziara yake barani Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, ambapo pamoja na mambo mengine atauzungumzia mzozo wa Mali.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John KerryPicha: picture-alliance/dpa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry mwishoni mwa juma hili anatarajiwa kuanza ziara yake katika mataifa tisa ya Ulaya pamoja na Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, ambapo pamoja na mambo mengine atauzungumzia mzozo wa Mali.

Ziara hiyo ya kwanza kufanywa na John Kerry tangu achukue wadhfa huo itamfikisha hadi Ufaransa, Italia, Uingereza na Ujerumani. Akiwa nchini Ufaransa, Kerry atakuwa na mazungumzo na waziri mwenzake, Laurent Fabius ambapo watauzungumzia mzozo wa Mali, mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati, mzozo wa Syria na mpango wa nyuklia wa Iran na Korea Kaskazini.

MUJAO wakiri kufanya shambulizi

Wakati Kerry akijiandaa kuuzungumzia mzozo wa Mali katika ziara yake hiyo, kundi la kigaidi la MUJAO ambalo ni tawi la mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, limekiri kuhusika na shambulizi lililotokea karibu na kambi ya makaazi ya wanajeshi wa Ufaransa kwenye mji wa Kidal nchini Mali.

Wapiganaji wa MUJAOPicha: AFP/Getty Images

Shambulio hilo limetokea wakati ambapo wanajeshi wa Mali na wale wa kimataifa wanapambana na hali tete kaskazini mwa Mali dhidi ya waasi wa Kiislamu. Ofisi ya gavana wa Kigali, imeeleza kuwa kiasi raia wawili wamejeruhiwa baada ya gari moja lilikuwa na mtu aliyejitoa mhanga kuripuka karibu na kambi ya wanajeshi wa Ufaransa na Chad na dreva huyo kuuawa.

Msemaji wa kundi la MUJAO, ambalo ni moja kati ya makundi ya waasi nchini Mali, Abu Walid Sahraoui amesema mashambulizi zaidi yatafanyika kuzunguka nchi hiyo. Sahraoui amesema kundi hilo limepeleka pia wapiganaji kwenye mji wa Gao. Amesema hawakupata ugumu wowote kuingia kwenye mji wa Kidal na kufanya shambulio hilo kama walivyopanga.

Mapigano yenye changamoto

Majeshi yanayoongozwa na Ufaransa yamekuwa yakikabiliwa na mapigano yenye mbinu za msituni kutoka kwa waasi tangu kuanza kwa operesheni ya kijeshi mwezi uliopita iliyosaidia kuwaondoa waasi kwenye miji ya Kaskazini ya Gao, Kidal na Timbuktu. Duru za jeshi zimesema kuwa mapambano yalianza usiku wa Jumatano kwenye mji wa Gao uliopo umbali wa kilometa 1,200 kutoka Bamako, baada ya waasi 40 kupenyeza na kuingia mjini humo.

Wanajeshi wa Ufaransa wakiwa GaoPicha: Reuters

Lakini Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian amesema majeshi ya Mali yakisaidiwa na yale ya Ufaransa yalifanikiwa kujibu mashambulizi. Akizungumza mjini Brussels, Ubelgiji, Le Drian amesema waasi watano wenye itikadi kali za Kiislamu waliuawa na wengine wawili walikamatwa.

Msemaji wa MUJAO, Sahraoui ameliambia shirika la habari la AFP kwamba waasi wanataka kuutwaa tena mji wa Gao na kwamba wapiganaji wao wamepewa amri ya kufanya mashambulizi. amesema iwapo maadui zao watakuwa imara zaidi, watarejea nyuma kwa ajili ya kujiimarisha hadi watakapoukomboa mji wa Gao.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW