Kerry kwa Syria: Kabidhi silaha za sumu uepuke kipigo
10 Septemba 2013Urusi imesema bado upo uwezekano wa kuusuluhisha mzozo wa Syria kwa njia ya mazungumzo, na kuitaka Marekani kuachana na mpango wake wa kuishambulia nchi hiyo kijeshi. Kauli hiyo ya Urusi imetolewa na waziri wake wa mambo ya nchi za nje Sergei Lavrov baada ya mazungumzo na mwenzake wa Syria Walid al-Mualem asubuhi ya leo mjini Moscow.
Sergei Lavrov, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, amesema wanasiasa wengi wanayo maoni sawa na yale ya Urusi, kwamba suluhisho la kijeshi katika mgogoro wa Syria litasababisha kusambaa kwa matendo ya kigaidi ndani ya Syria. Lavrov vile vile amesema kuwa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Syria yatazidisha tatizo la wakimbizi, na kuonya kuwa Urusi haiwezi kupuuza kitisho ambacho mashambulizi hayo yatasababisha kwa maisha ya raia wa Urusi wanaoishi Syria.
Syria tayari kwa mazungumzo yasio na masharti
Lavrov ambaye alikuwa amesimama pamoja na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Syria, Walid al-Mualem, amesema bado uwezekano wa kupatikana kwa suluhisho la kisiasa upo, huku akisisitiza kuwa amehakikishiwa na al-Mualem kwamba Serikali ya Syria ilikuwa tayari kwenda kwenye meza ya mazungumzo na wapinzani.
Waziri Walid Mualem amethibitisha msimamo wa serikali yake, akisema wako tayari kushiriki mazungumzo yaliyotarajiwa kufanyika mjini Geneva, bila masharti yoyote. Aidha, al-Mualem amesema serikali ya Syria inakaribisha mjadala na pande zote za kisiasa ambazo zinapenda amani irejee ndani ya nchi yao.
Hata hivyo, waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Syria amesema hali hiyo itabadilika kabisa, iwapo nchi hiyo itashambuliwa kijeshi.
Marekani yasema haiogopi vitisho vya Assad
Awali, rais wa Syria Bashar al-Assad alikaririwa na kituo cha televisheni cha kimarekani, CBS, akisema kuwa Marekani haina ushahidi wowote kuwa serikali yake iliamuru matumizi ya silaha za kemikali dhidi ya raia wake, na kuitolea changamoto kuuweka hadharani ushahidi huo kama kweli inao.
Hali kadhalika, CBS ilisema kuwa rais Assad aliionya Marekani, kuwa iwapo itaishambulia nchi yake, washirika wa serikali yake wanaweza kulipiza kisasi.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ambaye hivi sasa yuko ziarani mjini London, Uingereza, ameulizwa kuhusu kitisho hicho cha Rais Assad kujibu mashambulizi ya Marekani. Kerry amesema nchi yake haiwezi kutishika.
''Tunaishi katika dunia iliyojaa hatari, na kitisho hicho hakina tofauti yoyote na vingine vinavyotolewa kwetu kila siku. Tusipovikabili vitazidi kutolewa, na wanaovotoa wataamini kwamba wanaweza kumtisha yeyote.'' Amesema Kerry.
Syria yaombwa kukabidhi silaha za kemikali
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na mwenyeji wake, William Hague wa Uingereza, John Kerry amesema iwapo serikali ya Syria itakubali kukabidhi silaha zake za kemikali, hatua hiyo inaweza kuepusha mashambulizi.
Kerry alikwenda London baada ya mazungumzo na mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya nchini Lithuania, na pia mkutano na wajumbe wa Jumuiya ya nchi za kiarabu mjini Paris.
Katika mikutano hiyo, pande hizo, yaani Umoja wa Ulaya na Pia Jumuiya ya nchi za kiarabu ziliushutumua utawala wa rais Assad kwa matumizi ya silaha za kemikali zilizouwa raia, lakini hazikuunga mkono mashambulizi ya kijeshi yanayopangwa na Marekani.
Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFPE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman