Kerry, Netanyahu walaani mashambulizi Mashariki ya Kati
22 Oktoba 2015Viongozi hao wawili wamekutana mjini Berlin, na kulaani vikali mashambulizi hayo. Kerry alitoa wito wa kukomeshwa uchochezi wote na machafuko yote, lakini Netanyahu alirudia shutuma zake za awali za moja kwa moja kuwa Rais wa Palestina Mahmoud Abbas anapaswa kulaumiwa, akisema “anaeneza uwongo” kuhusu Israel na hadhi ya eneo takatifu ambalo ndilo kitovu cha mvutano.
Amesema kuwa Israel inahakikisha kuwa inabakisha hali ilivyo kwa sasa katika eneo hilo, ambalo linafahamika kwa Wayahudi kama Temple Mount, eneo takatifu kabisa la Uyahudi na makao ya Mahekalu ya biblia. Kwa Waislamu, ni mahali Patukufu, makao ya Msikiti wa Al-Aqsa, eneo la tatu tukufu katika Uislamu na ishara muhimu ya kitaifa kwa Wapalestina. Eneo hilo, lililonyakuliwa na Israel kutoka Jordan katika vita vya Mashariki ya kati mwaka wa 1967, hushuhudia machafuko ya mara kwa mara.
Wapalestina huishutumu Israel kwa kujaribu kubadilisha hali ilivyo ya muda mrefu katika eneo hilo, ambalo huwaruhusu Wayahudi kuzuru lakini siyo kufanya maombi. Netanyahu anakanusha hayo akisema kusitisha uchochezi ndiyo njia pekee ya kumaliza mvutano.
Kerry alionekana kuchukua tahadhari na hakumtaja Abbas kama wa kulaumiwa. Amesema na namnukuu, “tunapaswa kusitisha uchochezi, tunapaswa kusitisha machafuko” mwisho wa nukuu. Ameongeza kuwa amezungumza na Abbas na Mfalme Abdullah wa Jordan ambaye ana jukumu kusimamia eneo takatifu la Jerusalem, na wote wakamhakikishia kuwa kutakuwa na utulivu.
Kerry amesema anataka uwazi kuhusu hali ilivyo katika eneo hilo lakini maafisa wanasema haamini kuwa hilo linahitaji kuwekwa katika maandishi.
Baada ya kukutana na Netanyahu, Kerry kisha atamwona Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini. Kerry kisha atasafiri kesho kuelekea mjini Vienna, Austria, ambako atakutana na mawaziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Uturuki na Saudi Arabia kuujadili mzozo wa Syria. Kisha atazuru Amman, Jordan ambako atakutana na Mfalme Abdullah kabla ya kumalizia ziara yake nchini Saudi Arabia.
Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Hamidou Oummilkheir