1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry yuko Kenya kujadili usalama na ugaidi

Admin.WagnerD22 Agosti 2016

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani yuko Kenya kwa mazungumzo yanayotarajiwa kulenga masuala ya usalama wa kanda na ugaidi ukiwemo mzozo wa Sudan Kusini na yale yanayojiri nchini Somalia na Burundi wakati huu.

Picha: Reuters/E. Marcarian

Kerry amewasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi jana usiku na kupokelewa na waziri wa mambo ya nje wa Kenya Amina Mohamed hiyo ikiwa ni ziara yake ya pili nchini Kenya akiwa kama waziri wa mambo ya nje.

Msemaji wa ofisi ya rais nchini Kenya Manoah Esipisu amesema kwamba Kerry atakuwa na mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta juu ya usalama na utulivu wa kanda hiyo.

Amesema masuala mahsusi yatakayojumuishwa katika mazungumzo hayo ni kurudisha utulivu nchini Sudan Kusini kwa kujadili njia za kuzuwiya nchi hiyo isitumbukie tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, kuendeleza kipindi cha mpito cha kisiasa nchini Somalia na hali ya Burundi.

Kuinusuru Sudan Kuini

Akiwa mjini Nairobi atakutana na mawaziri wenzake wa mataifa manane ya Afrika kuijadili hayo.

Waasi wa SPLA Sudan Kusini.Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Patinkin

Kuhusiana na suala la mzozo wa Sudan Kusini afisa wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani amesema watu wa Sudan Kusini wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu na kuendelea kukosekana kwa utulivu nchini humo kumepelekea kuwepo kwa zaidi ya wakimbizi milioni moja na kuzuka kwa janga la kibinaadamu ambalo linapindukia hata uwezo wa jumuiya ya kimataifa kukabiliana nalo.

Jumuiya ya kimataifa imetumia mabilioni ya dola katika msaada kulisaidia taifa hilo changa kabisa duniani ambalo limejipatia uhuru wake hapo mwaka 2011. Uzalishaji wa mafuta ambao ndio chanzo kikuu cha mapato nchini humo umeshuka.

Somalia inakabiliwa na chaguzi muhimu za bunge mwezi ujao na uchaguzi wa rais hapo nwezi wa Oktoba.Kundi la al-Shabab lenye mafungamano na kundi la Al-Qaeda linaendelea kufanya mashambulio yanayosababisha maafa katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.

Burundi imekuwa kwenye machafuko tokea Rais Piere Nkurunziza ashinde muhula wa tatu ambapo upinzani wanasema ni kinyume na katiba.

Uchumi na rushwa nchini Nigeria

Kerry hapo kesho ataelekea nchini Nigeria ambapo atakuwa na mazungumzo na Rais Muhammadu Buhari kuhusu kuzorota kwa uchumi wa nchi hiyo na juhudi zake za kupambana na rushwa.

Abuja mji mkuu wa Nigeria.Picha: DW/K. Gänsler

Nigeria ni taifa lenye idadi kubwa kabisa ya watu barani Afrika wanaofikia milioni 160 na ni mojawapo ya mataifa yenye uchumi mkubwa barani barani Afrika.

Akiwa nchini Nigeria anatazamiwa pia kukutana na viongozi wa eneo la kaskazini mwa Nigeria linalokaliwa na Waislamu wengi ambapo kundi la Boko Haram linaendelea kufanya mashambulio yake.

Kundi la Boko Haram inaonekana kuwa limezongwa katika mapambano ya kuwania madaraka baada ya kutangazwa kwa kiongozi mpya kulikofanywa na kundi la Dola la Kiislamu mapema mwezi huu na kupingwa na kiongozi wa muda mrefu wa kundi hilo.

Mwandishi: Mohamed Dahman /Reuters/AP

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW