1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi dhidi ya Ecclestone kuendelea hadi Julai

14 Mei 2014

Shahidi mkuu katika kesi inayomkabili kiongozi wa mashindano ya Formula One, Bernie Ecclestone, anatarajiwa kuitwa tena mahakamani kutoa ushahidi wake mwishoni mwa mwezi wa Julai

Bernie Ecclestone München 2011 Gerichtstermin
Picha: Reuters

Mahakama moja ya Ujerumani imefanya uamuzi huo baada ya kumhoji Gerhard Gribkowsky, mtalaamu mmoja wa benki ambaye anatumikia kifungo gerezani kwa kupokea hongo.

Ecclestone, mwenye umri wa miaka 83, alikiri kumlipa Gribkowsky dola milioni 44 lakini akanusha kuwa kitita hicho kilikuwa ni hongo. Jaji anayeendesha kesi hiyo Peter Noll ameyasema hayo wakati akimwachia Gribkowsky baada ya siku tatu za kuwa kizimbani akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo. Shahidi huyo sasa atarejea mahakamani tena mnamo Julai 30.

Mawakili wa bwenyenye huyo wa F1 wamehoji tangu kuanza kwa kesi yake nchini Ujerumani kuwa Ecclestone alipeana pesa hizo kutokana na hofu na hakuwa na nafasi yoyote nzuri kumliko Gribkowsky, ambaye alikuwa afisa wa benki ya Bayern LB, iliyokuwa na hisa nyingi katika Formula One.

Gerhard Gribkowsky, anadaiwa kupokea hongo kutoka kwa Ecclestone, ataendelea kutoa ushahidi JulaiPicha: Getty Images

Waendesha mashitaka wamemfungulia mashitaka Ecclestone kwa kumhonga afisa wa umma na kuchochea matumizi mabaya ya fedha. Wanasema lengo la kutoa hela hizo lilikuwa ni kuhakikisha kuwa kampuni yenye makao yake jijini London ya CVC, ambayo Ecclestone aliitaka iwe mwekezaji mkuu, inapata udhibiti wa F1, mchezo ambao ni wenye utajiri mkubwa sana ulimwenguni.

Gribkowsky mwenye umri wa miaka 56 anasisitiza kuwa Ecclestone alikuwa na wasiwasi kuwa angepoteza kazi yake inayomlipa hela nyingi, kama Afisa Mkuu Mtendaji wa mchezo wa Formula One kama mwekezaji mwengine angechukua usukani.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef