1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi kubwa dhidi ya Mafia kuanza Italia

13 Januari 2021

Washukiwa 350 wa kundi hatari la mafia linaloitwa Ndrangheta wanashtakiwa kwenye kesi hiyo ya kwanza kushuhudiwa katika kipindi cha miongo kadhaa nchini Italia. Ndrangheta ni kundi lililoingia kwenye mabara yote ya dunia

Italien Maxi-Operation gegen Ndrangheta Mafia  Polizei Video
Picha: Comando Generale Carabinieri/dpa/picture alliance

Italia leo inashuhudia kesi kubwa kabisa dhidi ya watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi hatari la mafia la Ndrangheta. Hii ni kesi kubwa nchini humo ambayo haijawahi kutokea kwa kipindi cha miongo kadhaa.

Kesi hiyo ya aina yake inayotarajiwa kufunguliwa muda wowote leo Jumatano huko kusini mwa Italia inawahusisha watu 350 wanaoshukiwa kuwa ni wanachama wa kundi la mafia la Ndrangheta pamoja na wafuasi wao na inatarajia kuendeshwa kwa kipindi cha hadi miaka miwili.

Mashtaka 

Hii ni kesi kubwa kabisa nchini Italia ikionesha juhudi za serikali za kuiandama mitandao ya uhalifu nchini humo. Washukiwa wanakabiliwa na mashtaka kadhaa ikiwemo kufungamana au kuwa wanachama wa kundi la Mafia,mauaji,umiliki wa silaha kinyume na sheria, usafirishaji wa madawa ya kulevya,kujipatia fedha kwa njia za mabavu pamoja na utoaji mikopo kwa kiwango kikubwa cha riba. Mwendesha mashtaka wa kesi za kukabiliana na Mafia katika mkoa wa Calabria, Italia Nicola Gratteri anasema.

''Wataalamu wanakubaliana kwamba Ndrangheta ndio kundi hatari la Mafia liko kwenye mabara yote. Ni kundi lenye utajiri mkubwa kabisa kwa sababu linashikilia takriban peke yake, biashara ya kusafirisha Cocaine barani Ulaya''

Kesi itafanyika kwenye jengo hiliPicha: Gianluca Chininea/AFP/Getty Images

Mashahidi kiasi 900 wanatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hii wakiwemo waliowahi kuwa wanachama wa mtandao huo wa Mafia ambao wanatarajiwa kukiuka kiapo cha Mafia cha kutakiwa kukaa kimya au kutotowa siri za ndani za kundi.

Aidha kesi hiyo haitoendeshwa kwenye mahakama za kawaida bali itafanyika katika jengo maalum lililojengwa katika mji wa Lamezia Terme. Na kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Italia watuhumiwa wengine 90 zaidi wanaoshtakiwa wameamua kusimama kwenye kesi itakayowapa nafasi au haki ya kuamua kezi zao zisikilizwe kwenye mahakama ipi ya nchi, kesi hiyo itaanza Januari 27.

Msako

Itakumbukwa kwamba kesi hizi zinakuja baada ya mnamo mwezi Desemba mwaka 2019 maafisa wa Carabinieri kuwakamata zaidi ya washukiwa 300 wanaoshukiwa kuwa wanachama wa Mafia katika mojawapo ya msako mkubwa kabisa uliowahi kufanyika tangu miaka ya 1980 ukiyalenga makundi hayo ya uhalifu.

Picha: picture-alliance/Ropi

Na miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na wanasiasa,mawakili pamoja na wafanyabiashara wa Italia. Msako huo ulifanyika pia kwenye nchi nyingine kama Bulgaria na Ujerumani pamoja na Uswisi.Mwendesha mashtaka Nicola Gratteri anasema sheria za kupambana na mafia zinahitajika kote ulaya kutokana na uhalisia uliopo.

Mkoa wa Calabria ulioko kusini mwa Italia ambako kuna umasikini mkubwa ndiko makaamu hasa ya kihistoria ya kundi hatari la Mafia la Ndrangheta, hili ni kundi mojawapo kubwa kabisa na lenye nguvu duniani linalopanga uhalifu.

Lakini kwa kipindi kirefu kundi hilo pia limejigawa kutoka Calabria na kuingia hadi Australia, nchi nyingine nyingi za barani Ulaya na Amerika ya Kaskazini likitajwa kuwa ni kundi linaloongoza katika uingizaji wa Cocaine barani Ulaya.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW