1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Dominic Ongwen na Vipodozi Magazetini

Oumilkheir Hamidou
9 Desemba 2016

Kufikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu mjini The Hague, ICC, kamanda wa zamani wa wanamgambo wa Uganda Lord Resistance Army, Dominik Ongwen, na kichaa cha kujichubua ngozi ni miongoni mwa mada magazetini

Niederlande Dominic Ongwen vor dem  Internationalen Strafgerichtshof
Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Dejong

Tuanze lakini na kesi ya aliyekuwa kamanda wa kundi katili miongoni mwa makundi katili ya wanamgambo barani Afrika: Dominic Ongwen aliyefikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu mjini The Hague. "Orodha ya visa vya kikatili ni ndefu kupita kiasi" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la mjini Münich "Süddeutsche Zeitung". Gazeti hilo limeorodhesha visa vya mauwaji, mateso, ubakaji na watu kugeuzwa watumwa ambavyo Ongwen anabidi ajieleze mbele ya mahakama hiyo ya kimataifa. Dominic Ongwen na kundi lake la waasi la Lord Resistance Army anatuhumiwa kuhusika na mauwaji ya watu zaidi ya laki moja tangu mwaka 1987 na kuwateka nyara maelfu ya watoto. Anabidi ajibu mashitaka kuhusiana na uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinaadam katika kadhia 70 zilizotokea kati ya mwaka 2002 na 2005 kaskazini mwa Uganda. Süddeutsche Zeitung linaelezea jinsi kesi hiyo ilivyofunguliwa kwa kuonyeshwa kanda za video na picha za miili ya watu iliyokatwa vipande vipande.

 

Limemnukuu mwendesha mashitaka mkuu Fatou Bensouda akimtaja Ongwen kuwa " katili na mbakaji" na kwamba miongoni mwa wenye kuamrisha katika kundi hilo la waasi,"yeye ndie aliyekuwa habithi kuliko wote." Visa vilivyotajwa hajakanusha kua vimetokea,anadai lakini vimefanywa na LRA na sio yeye. Na ameapa kwa jina la Mungu akisema yeye hahusiki. Usumbufu na mateso aliyo yapata alipotekwa nyara akiwa mdogo nayo pia hayasaidii kitu. Kesi dhidi ya Ongwen inafuatiliziwa kwa makini nchini mwake Uganda ambako Süddeutsche limekusanya maoni ya wahanga wanaosema pindi Ongwen akisamehewa, na kurejeshwa Uganda, basi wao wenyewe watamhukumu.

 

Korti ya ICC yatuhumiwa kuwalenga waafrika tu

 

Mtihani unaoikaba mahakama hiyo ya kimataifa ICC mjini The Hague nao pia umemulikwa kwa mara nyengine tena wiki hii na wahariri wa magazeti ya Ujerumani. Lilikuwa gazeti la "Neues Deutschland" lililozungumzia "mzozo mjini The Hague" pamoja na lawama dhidi ya taasisi hiyo ya kimataifa. Gazeti hilo linazungumzia kizungumkuti kikubwa kinachomkabili mwenyekiti wa mahakama hiyo ya kimataifa ya ICC, bibi Silvia Fernandez de Gurmendi wa Argentina baada ya mataifa kadhaa ya Afrika, pamoja  pia na Urusi kutangaza kubatilisha mkataba wa Rome uliopelekea kuundwa mahakama hiyo mwaka 1998. Baada ya kuelezea visa vya uhalifu vinavyoandamwa na mahakama hiyo tangu ilipoanza shughuli zake julai mosi mwaka 2002, Neues Deutschland linasema hivi sasa ICC inakosolewa kugeuka chombo cha wakoloni wa zamani, kwa kuwa pekee waafrika ndio walioandamwa hadi sasa.

 

Hoja hizo, linaendelea kuandika gazeti la Neues Deutschland, ndio sababu iliyomfanya mwendesha mashitaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda ambae binafsi anatokea Gambia, kutangaza kuchunguza visa vya uhalifu wa vita vilivyotokea pia Afghanistan wakituhumiwa wanajeshi wa Marekani na shirika la ujasusi la Marekani CIA. Neues Deuchland limekumbusha wito uliotolewa na mwenyekiti wa halmashauri ya haki za binaadam ya umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Husein, katika mkutano wa hivi karibuni wa mataifa 124 yaliyotia saini makubaliano ya Roma, wa kuungwa mkono zaidi korti ya ICC.

 

Binaadam haridhiki na alichopewa na Mungu

 

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inamulika jinsi ambavyo binaadam haridhiki na alichojaaliwa na Mungu. "Kichaa cha kujichubua ngozi" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la "Der Tagesspiegel" linalozungumzia jinsi wanawake wengi wa Afrika kusini walivyoingia mbioni  na kutumia kila wanachokisikia ili kubadilisha rangi yao ya ngozi: Hata kama ni hatari kwa afya zao linaandika gazeti hilo linalolinganisha kiu hicho na ile hali kwamba katika nchi za ulaya rangi iliyokoza ya mwili  ndio inayoangaliwa kuwa ya kupendeza.

 

Mwandishi: Hamidou Oumilkheir/BASIS/PRESSEM/ALL/PRESSE

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW