1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Felicien Kabuga kuanza Alhamisi (29.09.2022)

29 Septemba 2022

Felicien Kabuga ni mmoja mwa watu wa mwisho kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda. Kesi hiyo inaanza bila ya Mtuhumiwa kuhudhuria.

Ruanda Der Geschäftsmann Felicien Kabuga
Picha: Simon Wohlfahrt/AFP

Majaji katika mahakama moja ya Umoja wa Mataifa mjini The Hague nchini Uholanzi, wamesema leo kuwa Felicien Kabuga raia wa Rwanda mwenye umri wa miaka 87 na anayetuhumiwa kuchochea mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini humo hatahudhuria ufunguzi wa kesi dhidi yake kwa makosa matatu ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda, lakini imeamua kuwa kesi hiyo itaendelea.

Felicien Kabuga ni mmoja mwa watu wa mwisho kukamatwa kwa kosa la mauaji ya kimbari na kufikishwa mahakamani na kuanza kwa kesi yake kunaashiria siku muhimu kwa Wanyarwanda walionusurika mauaji hayo au wale ambao familia zao ziliuawa katika mauaji ya siku 100 yaliyosababisha vifo vya watu laki nane.

Jaji Kiongozi Iain Bonomy amesema kesi hiyo inaweza kuanza bila uwepo wa Kabuga, ambaye hakuhudhuria kutokana na mzozo kuhusu haki yake ya kuwakilishwa.

Soma zaidi: Kabuga mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari Rwanda afikishwa mahakama ya The Hague

Mawakili wakihudhuria kesi ya Felicien Kabuga mjini The Hague, UholanziPicha: Koen van Weel/REUTERS

Kutohudhuria ni uamuzi wa kimkakati

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama hiyo, Serge Brammertz, amesema kitendo cha Kabuga kutohudhuria ni "uamuzi wa kimkakati".

Brammertz ameendelea kuwa katika kipindi chote cha maandalizi ya kesi hiyo, Kabuga alikuwa na wakili ambaye ni mwanasheria hodari kuweza kumwakilisha, na kusisitiza kuwa kwa upande wao, mchakato wa kesi hiyo ni wa uhakika kabisa.

Brammertz amesema kesi hiyo ni muhimu baada ya haki kusubiriwa kwa muda mrefu. Baadhi ya mashahidi 50 watatoa ushuhuda wao kwa upande wa mashtaka.

Mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi walio wachache nchini Rwanda yalianza Aprili 6, 1994, wakati ndege iliyombeba Rais wa wakati huo, Juvenal Habyarimana ilipodunguliwa na kuanguka katika mji mkuu, Kigali, na kumuua kiongozi kutoka kabila la Wahutu walio wengi nchini Rwanda. Ifahamike kwamba Binti wa Kabuga aliolewa na mtoto wa Habyarimana.

Soma zaidi:Kabuga atafikishwa kizimbani Septemba 29

Jamii ya walio wachache ya Watutsi walilaumiwa kwa kuidungua ndege hiyo ambayo alikuwemo pia Rais wa Burundi wa wakati huo, Cyprien Ntaryamira.

Mchoro wa Felicien Kabuga akiwa katika Mahakama moja nchini Ufaransa Mei 20, 2020Picha: Benoit Peyrucq/dpa/AFP/picture alliance

Kabuga mwenye shauku ya mauaji

Katika maelezo yake ya ufunguzi, wakili wa upande wa mashtaka Rashid Rashid amemuelezea Kabuga kuwa mfuasi mwenye shauku ya mauaji na ambaye alitoa msaada wa silaha, mafunzo na kuwatia moyo wanamgambo wa Kihutu  wanaojulikana kama Interahamwe.

Naphtal Ahishakiye, katibu mtendaji wa kundi la manusura wa mauaji hayo ya kimbari linalojulikana kama Ibuka, amesema kuwa bado hakujachelewa kwa haki kutendeka. Ahishakiye ameongeza kuwa hata kwa pesa na ulinzi, mtu hawezi kuepuka uhalifu wa mauaji ya kimbari.

Soma zaidi: Wanyarwanda wataka Kabuga ashtakiwe nyumbani

Kabuga anashtakiwa kwa mauaji ya kimbari, uchochezi wa mauaji ya kimbari, njama za kufanya mauaji pamoja na mateso na maangamizi. Licha ya kukana mashtaka hayo, Felicien Kabuga aliyekamatwa karibu na mjini Paris, Ufaransa mwaka 2020, endapo akipatikana na hatia atakabiliwa na adhabu ya juu zaidi ya kifungo cha maisha jela.

(APE)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW