Kesi ya Hariri yaanza
16 Januari 2014Watuhumiwa wote wanne kwenye kesi hiyo ni raia wa Lebanon na hawakuwapo mahakamani wakati kesi yao ikitajwa.
Kesi dhidi ya mtuhumiwa wa tano, pia raia wa Lebanon, anayetuhumiwa kushiriki kwa mpango huo wa mauaji ya Hariri, inatazamiwa kusikilizwa katika siku zijazo.
Watuhumiwa wote watano wanaaminika kuwa na mafungamano na kundi la Hizbullah, ambalo limekuwa na mahusiano ya karibu na utawala wa Syria.
Mwendesha Mashitaka, Norman Farell, alisema kwamba mshambuliaji wa kujitoa muhanga akiwa na miripuko yenye uzito wa kati ya kilo 2,500 na 3,000 ndiye aliyemuuza Hariri tarehe 14 Februari mwaka 2005.
Mshambuliaji huyo alitambulika baadaye kupitia mabaki ya meno yake.
Picha za mashambulizi zaoneshwa
Upande wa mashitaka uliionesha mahakama picha za kamera za siri ambapo gari jeupe linaonekana likiingia kwenye eneo muda mfupi kabla ya msafara wa Hariri kupita.
Farell alisema nguvu za mripuko huo zilimrusha Hariri nje ya gari yake, akiogeza kwamba dereva lazima ndiye aliyekuwa mshambuliaji wa kujitoa muhanga kwani gari ilikuwa ikiendelea kutembea wakati iliporipuka.
Kwa mujibu wa Farell, washukiwa wawili wakuu, Mustafa Baderddine na Salim Ayash, waliiandaa operesheni hiyo kwa miezi minne kabla huku wakichunguza mienendo yote ya Hariri kwa miezi mitatu.
Mtoto wa kiume wa Hariri, na ambaye pia alikuwa waziri mkuu wa Lebanon, Saad Hariri, alikuwapo wakati wa kesi hiyo, na alipangiwa kuzungumza kutoa ushahidi wake.
Ni mauaji haya ya Rafik Hariri, ambayo yalichochea upinzani mkali na maandamano kwenye mitaa kadhaa nchini Lebanon, na hivyo kuishinikiza Syria kuondosha wanajeshi wake kutoka nchi hiyo baada ya kuwapo kwa miaka 29 mfululizo.
Mahakama hiyo maalum kwa ajili ya Lebanon ilianzishwa mwaka 2009 na Umoja wa Mataifa na imekuwa chanzo cha mzozo kati ya vyama hasimu vya kisiasa nchini humo, ambako Hizbullah imetuma wanajeshi wake kuunga mkono utawala wa Assad na vyama vya Kisunni vinakasirishwa na uamuzi huo.
Mashambulizi dhidi ya ngome ya Hizbullah
Matokeo ya hatua hiyo ya Hizbullah, ni kuvishuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria vikipiganwa hadi kwenye mitaa ya Lebanon.
Hivi leo, mshambuliaji wa kujitoa muhanga ameliripua gari lake katika uwanja mkuu wa Hermel, kiliko kikosi cha kijeshi cha Hizbullah kwenye Bonde la Bekaa, na kuwauwa watu watatu.
Haya ni mashambulizi ya kwanza kwenye mji huo, ingawa ni ya tano kwenye ngome za Hizbullah tangu kundi hilo kukiri kwamba inapigana upande wa Rais Assad kwenye vita vya Syria.
Waziri wa Afya wa Lebanon, Ali Hassan Khalil, amesema pamoja na watu hao watatu waliouwawa, mashambulizi hayo yamewajeruhi pia watu wengine 30.
Mpigapicha wa shirika la habari la AFP, ameelezea kuona vipande vya miili ya watu vilivyotapakaa kwenye eneo la tukio.
Jengo lililolengwa kwenye mashambulizi haya lina ofisi kadhaa za serikali, na Rais Michel Suleiman ameyaita mashambulizi hayo kuwa ni sehemu ya "mkururo wa matendo ya kihalifu yanayokusudiwa kuisambaratisha Lebanon."
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf