Kesi ya jaribio la 'mapinduzi' yaanza kusilikzwa Kongo
7 Juni 2024Kesi hiyo ilianza kusikilizwa katika saa za asubuhi siku ya Ijumaa mbele ya mahakama ya kijeshi iliyoko ndani ya jela ya kijeshi ya Ndolo katika mji mkuu Kinshasa, kwa mujibu wa shirika la habari la Ufaransa AFP.
Soma pia:Marekani: Kongo haijatoa maelezo kukamatwa kwa raia wetu
Washtakiwa hao waliowajumuisha wanawake wanne waliingia kizimbani wakiwa wamevalia sare za magereza za rangi ya samawati na njano.
Wanadiplomasia wa magharibi, waandishi habari na mawakili, pia walihudhuria kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Washambuliaji walikuwa raia wa mataifa kadhaa
Msemaji wa jeshi la Kongo jenerali Sylvain Ekenge, amesema njama hiyo inayodaiwa iliongozwa na Christian Malanga, raia wa Marekani mwenye asili ya Kongo ambaye aliuawa na vikosi vya usalama.
Soma pia:DRC yamtaja mmarekani mmoja aliyehusika katika jaribio la kuipindua serikali
Ekenge amesema washambuliaji hao walikuwa raia wa mataifa kadhaa na kwamba takriban 40 kati yao walikamatwa na wengine wanne ikiwa ni pamoja na Malanga kuuawa.
Sababu ya tukio hilo bado haijafahamika, lakini serikali ilililaani na kulitaja kuwa "jaribio la kuvuruga taasisi". Hati ya mahakama inaonyesha kuwa washitakiwa 53 wanahukumiwa akiwemo Christian Malanga ijapokuwa amefariki dunia.
Soma pia:Umoja wa Afrika wakosoa jaribio la mapinduzi lililotokea DR Congo
Mwanawe, ambaye ni Mmarekani, pamoja na raia wengine wawili wa Marekani pia wanakabiliwa na mashtaka hayo. Raia mmoja wa Ubelgiji mwenye asili ya Kongo pia ni miongoni mwa washtakiwa hao.
Orodha ya mashtaka ya kesi ya jaribio la 'mapinduzi'
Kulingana na hati hiyo ya mahakama, mashtaka katika kesi hiyo yanajumuisha mashambulizi, ugaidi, kumiliki silaha na zana za kivita kinyume cha sheria, jaribio la kuua, kujihusisha na uhalifu, mauaji na kufadhili ugaidi.
Uchunguzi wafanywa juu ya mauaji ya kiholela
Uchunguzi tofauti unafanywa kuhusu mauaji ya kiholela yanayodaiwa kufanywa na wanajeshi baada ya operesheni hiyo.
Watu wenye silaha wafanya mashambulizi
Watu wenye silaha walishambulia nyumba ya waziri wa uchumi Vital Kamerhekatika saa za mapema mnamo Mei 19 kabla ya kuelekea eneo la karibu la Palais de la Nation ambalo lina ofisi za Rais Felix Tshisekedi.
Baadaye jeshi hilo lilitangaza kwenye televisheni ya taifa kwamba vikosi vya usalama vimetibua "jaribio la mapinduzi".