1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Manafort ni mtihani kwa Mueller

31 Julai 2018

Manafort akabiliwa na mashtaka 18 ya udanganyifu na njama za wizi wa kibenki akituhumiwa kupokea mamilioni ya dolla nchini Ukraine na kuzificha kwenye benki za nje bila kuzilipia kodi Marekani

USA - Donald Trump und Paul Manafort
Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS/M. Reinstein

Aliyekuwa mwenyekiti wa kampeini ya urais ya Donald Trump katika uchaguzi wa mwaka 2016 Paul Manafort anakabiliwa na mashtaka 18 ya uhalifu katika kesi inayosikilizwa katika mahakama ya jimbo la Virginia mjini Alexandria nchini Marekani. Kesi hiyo inaanza leo. Manafort amekanusha mashtaka yote.

Nusu ya mashtaka yanayomkabili Manafort yanahusiana na njama za udanganyifu na wizi wa kibenki makosa ambayo yanabeba kifungo cha hadi miaka 30 jela kwa kila kosa ijapokuwa inawezekana ikiwa atakutwa na hatia kukabiliwa na hukumu ndogo kiasi kwa kuzingatia kanuni au taratibu za mahakama. Ikiwa atakutwa na hatia ya kuhusika na makosa yote 18 yanayomuandama Manafort mwenye umri wa miaka 69 huenda akakabiliwa na kifungo cha miaka 7 hadi 12 jela kwa mujibu wa taratibu za kimahakama anasema Tess Lopez ambaye ni mtaalamu wa masuala yanayohusu hukumu kutoka Carlifonia.

Lopez anasema kwamba majaji sio siku zote wanatoa hukumu ndani ya utaratibu uliopo na huenda pia wakatoa uamuzi kutokana na mazingira ya makosa yanayotajwa. Justin Papemy mwasisi mwenza wa shirika la wataalamu wa masuala ya magereza linalojulikana kama Prison Professors anakadiria kwamba Manafort huenda ikitokea ameshtakiwa kwa makosa yote yanayomkabili,akafungwa kifungo cha miaka minane hadi 10 kwa mujibu wa kanuni zilizopo.

Kesi inayohusika na wizi wa kibenki na ugandanyifu katika masuala ya kodi itakuwa ni mtihani wa kwanza utakaoonesha uwezo wa Mueller na tume yake katika kumshtaki msaidizi huyo wa zamani wa rais Trump. Wasaidizi wengine watatu wa Trump akiwemo mshirika wa muda mrefu wa kibiashara wa Manafort Rick Gates wamekiri mashtaka na wanashirikiana na tume ya uchunguzi ya Mueller. Rais Trump amejikuta katika njia panda kati ya kuonesha kumuunga mkono  Manafort  na kujaribu kutojihusisha nae.Manafort ni mtu aliyeendesha kampeini ya Trump ya kuwania urais kwa miezi mitatu na kuhudhuria mkutano uliofanyika mwezi Juni mwaka 2016 katika jumba la Trump Tower uliofanyika kati yake na warusi mkutano ambao unamulikwa katika uchunguzi unaoendeshwa na jopo la Mueller kuhusiana na uwezekano wa kuhusika kwa serikali ya Urusi katika kampeini za Trump.

Rick GatesPicha: picture-alliance/dpa/AP/S. Walsh/AP

Kukutwa na hatia kwa Manafort kutatoa mwamko kwa tume ya Mueller ambaye amewashtaki au kuwatuhumu watu 32 na makampuni matatu tangu alipoanzisha uchunguzi wake miezi 14 iliyopita.Lakini pia kufutiliwa mbali kwa kesi dhidi ya Manafort ni hatua itakayotoa fursa ya kuungwa mkono juhudi za Trump na washirika wake za kutaka kuonesha kwamba uchunguzi huo wa Mueller hauna maana isipokuwa ni hatua ya kumtafuta mchawi na inayopoteza rasilimali za nchi.

Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Trump hadi sasa anakanusha kwamba hahusiki kwa namna yoyote. Manafort anatuhumiwa kwamba ameficha kiasi kikubwa cha dolla milioni 60 katika akaunti kwenye benki ambazo hazijulikani nje ya nchi alizopokea nchini Ukraine na alikwepa kuzilipia kodi.Waendesha mashtaka pia wanamtuhumu Manafort kwa kuzidanganya benki za Marekani ili kujipatia mikopo ya ujenzi wa majumba katika harakati zake za kutaka kuendelea kuishi maisha ya anasa baada ya mteja wake rais wa zamani wa Ukraine anayeegemea upande wa Urusi Viktor Yanukovich alipoangushwa madarakani mwaka 2014 na mtiririko wa fedha kukauka.Hata hivyo Manafort anakanusha makosa yote.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Iddi SseSsanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW