1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Kesi ya mashambulizi ya Paris 2015 yaanza

8 Septemba 2021

Watu 20 wanaotuhumiwa kwa mashambulizi ya mwaka 2015 yaliyouwa watu 130 na kuwajeruhi wengine kadhaa jijini Paris wamepandishwa kizimbani katika kesi inayotazamiwa kuwa ya aina yake nchini Ufaransa.

Frankreich | Prozessauftakt zum Pariser Terroranschlag vom November 2015
Picha: Thibault Camus/AP/picture alliance

Katika jengo kongwe la karne ya 13, chumba cha mahakama kilijaa siku ya Jumatano (Septemba 8) mjini Paris, pale Salah Abdeslam alipokuwa wa kwanza kujitambulisha na ambaye baada ya kutamka jina la Mungu alitangaza kwamba yeye ni mpiganaji wa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu.

Jaji anayesimamia kesi hiyo, Jean-Louis Peries, alielezea kutambua jinsi mazingira ya matukio ya usiku wa tarehe 13 Novemba 2015 yasivyokuwa ya kawaida na kesi hii ambayo inatazamiwa kuchukuwa miezi tisa.

"Matukio hayo ambayo ndiyo tunaelekea kuamua juu yake yameandikwa kwa uzito wake wa kihistoria kama moja ya matukio ya kimataifa na kitaifa kwa karne hii," alisema jaji huyo.

Zaidi ya mawakili 300 wanahusika kwenye kesi hii kutoka pande zote mbili. Abdeslam ndiye mshambuliaji pekee aliyebakia hai kwenye mashambulizi hayo na ndiye pekee anayeshitakiwa kwa mauaji hayo.

Mtandao huo huo wa magaidi ulihusika na mashambulizi mengine mjini Brussels miezi michache baadaye ambayo yaliuwa watu 32.

Kesi dhidi ya watu 20 waliofanya mauaji ya watu 130 na kujeruhi mamia ya mengine mwezi Novemba 2015 imeanza mjini Paris.Picha: Thibault Camus/AP/picture alliance

Dominique Kelelemoes, ambaye mtoto wake wa kiume aliuawa kwenye moja ya mikahawa iliyoshambuliwa siku hiyo, alisema mwezi mmoja uliotengwa kwa ajili ya ushahidi wa wahanga utakuwa muhimu kwa kujiponya wao wenyewe na kuliponya taifa.

Baba huyo aliliambia shirika la habari akiwa mahamakani hapa leo kwamba magaidi waliporusha risasi zao walidhani kwamba wanaushambulia umma, lakini haukuwa umma, bali watu wa kawaida waliokuwa na maisha yao, waliokuwa na mapenzi na matumaini, na kwamba hilo ndilo jambo muhimu analotaka kulisema kwenye chumba cha mahakama.

Washitakiwa sita hawapo kizimbani

Ingawa watu 20 wanashitakiwa kwenye kesi hii, sita kati yao wanashitakiwa wakiwa hawapo mahakamani. Abdeslam, ambaye aliliacha gari lake la kukodi kaskazini na mkanda wa kujiripulia ambao haukuwa ukifanya tena kazi na kukimbilia kwao Brussels, amekataa kuzungumza na waendesha mashitaka.

Philippe Duperron, mmoja wa wazazi ambaye watoto wao waliouawa kwenye mashambulizi ya Novemba 2015.Picha: Michel Euler/AP/picture alliance

Kwa kuwa yeye ndiye anayetajwa kama mtu mwenye majibu kwa sehemu kubwa ya maswali yaliyosalia juu ya mashambulizi na watu walioyapanga barani Ulaya na hata nje ya Ulaya, atalazimika kuhojiwa mara kadhaa kizimbani.

Kwa mara ya kwanza, wahanga wanaweza pia kusikiliza moja kwa moja jinsi kesi ilivyokwenda wakiwa majumbani kwao, nusu saa baada ya kesi kuanza.

Kesi hii inatazamiwa kuendelea kwa miezi tisa, ambapo mwezi huu wa Septemba umepangiwa uwe wa kuonesha ushahidi wa polisi na wapelelezi.

Mwezi ujao wa Oktoba utatengwa kwa ajili ya wahanga kutoa ushahidi wao, ambapo kutoka Novemba hadi Disemba, maafisa akiwemo rais wa zamani, Francois Hollande, watatowa ushahidi wao, na pia jamaa za washambuliaji.

Mashambulizi haya yanatajwa kuibadilisha sana Ufaransa, kwani baada ya hapo ndipo ilipotangazwa sheria hali ya hatari na sasa kumekuwa na maafisa wa usalama wenye silaha muda wote wakilinda maeneo ya umma.  

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW