Kesi ya mauaji ya Kunduz yatupwa Bonn
12 Desemba 2013Shambulio hilo liliitishwa na kamandi ya Ujerumani katika vikosi vya Jumuiya ya kujihami NATO jimboni Kunduz. Zaidi ya watu 100 waliuawa katika shambulio hilo, ambalo bunge la Ujerumani lilielezea kuwa ni baya zaidi lililohusisha jeshi la Ujerumani tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia.
Karibu miezi tisa tangu kuanza kwa kesi hiyo, na zaidi ya miaka minne tangu kutokea kwa mashambulizi dhidi ya malori mawili ya kubeba mafuta, hukumu imetolewa jana Jumatano, ambapo jaji aliesikiliza kesi hiyo Heinz Sonneberger alitangaza kuwa kamanda wa Ujerumani alieitisha mashambulizi hayo Kanali Georg Klein hakufanya hivyo kutokana na uzembe, na hivyo kutupilia mbali madai hayo.
Hakukiuka sheria za kimataifa
Katika hukumu yake, jaji Sonneberger alisema mahakama imeshawishika kwamba katika kuamrisha shambulio hilo, kamanda Klein hakukiuka taratibu za sheria za kimataifa za kuwalinda raia. Jaji huyo aliongeza kuwa Klein aliyabaini kwa usahihi malori hayo ya mafuta kama vifaa vya kijeshi, na kwamba kutokana na mafuta yaliyokuwa yameyabeba, yalikuwa ya muhimu kwa shughuli za usafirishaji wa Wataliban, na yangetumika katika shambulizi.
Mahakama ilisema inaamini kamanda Klein alifanya uhakiki wa kutosha, akiwawuliza watoa taarifa waliokuwepo eneo la tukio mara saba, iwapo kulikuwepo na raia, na kila mara aliambiwa hawakuwepo.
Muhimu kwa wanajeshi
"Hukumu hii ni muhimu kwa serikali na kwa wanajeshi pia. Pamoja na hatari za kimwili zinazowakabili huko katika uwanja wa vita, zimeongezeka pia hatari nyingine za kisheria. Kupitia hukumu hii wanaweza kujiskia angalau salama," alisema Mark Zimmer, wakili wa upande wa serikali katika kesi hii.
Kwa upande wake, wakili wa upande wa mashtaka Karim Popal alisema watakataa rufaa, na kuongeza kuwa hukumu hiyo haikuwa ya haki, na kwamba familia za wahanga wa mashambulizi hayo zimesononeshwa.
Moja wa watu wawili waliofungua madai hayo Abdul Hanan ambaye alipoteza watoto wake wawili katika mashambulizi hayo, aliiambia DW kuwa amesikitishwa na matokeo ya kesi hiyo."Tunataka huyu Georg Klein pamoja na marubani wote waadhibiwe. Tulishambuliwa pasipo na sababu zozote za msingi na tukawuliwa wapendwa wetu," alisema.
Kilichotokea
Kamanda Klein aliziita ndege za kivita za Marekani kuyashambulia malori mawili ya mafuta kaskazini mwa mji wa Kunduz, ambayo NATO iliamini yalikuwa yametekwa na waasi wa kundi la Talibani. Serikali ya Afghanistan ilsiema watu 99, wakiwemo raia 30 waliuawa katika shambulio hilo. Lakini makundi huru ya haki za binaadamu yalisema kati ya raia 60 na 70 waliuawa.
Idadi kubwa ya vifo vilivyotokana na shambulizi hilo viliitikisa Ujerumani, na kumlaazimisha waziri wake wa ulinzi wakati huo kujiuzulu, kwa madai kwamba alificha idadi sahihi ya wahanga wa kiraia wa shambulio hilo, katika wiki za kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2009.
Hukumu hii ilitolewa siku ambapo mshambuliaji wa kujitoa mhanga aliushambulia msafara wa wanajeshi wa Ujerumani karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul, lakini hakukuripotiwa maafa yoyote.
Mwandishi: Bleiker Carla/HDG-DE
Iddi Ismail Ssessanga/rtre,afpe.
Mhariri: Daniel Gakuba