1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya mauaji ya Thomas Sankara yaanza Ougadougou

11 Oktoba 2021

Watu 14 akiwemo rais wa zamani Blaise Compaore wanashtumiwa kuhusika na mauaji ya kiongozi huyo aliyekuwa na ushawishi mkubwa na alieuliwa kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya 1987.

Burkina Faso Präsident Thomas Sankara
Picha: picture-alliance/dpa

Kesi ya mauaji ya kiongozi wa zamani wa Burkina Faso Thomas Sankara imeanza kusikilizwa leo na mahakama ya kijeshi ambapo watu 14 akiwemo rais wa zamani Blaise Compaore wanashtumiwa kuhusika na mauaji ya kiongozi huyo aliyekuwa na ushawishi mkubwa na alieondolewa madarakani na Compaore katika mapinduzi ya mwaka 1987.

Kwa mujibu wa nyaraka za jeshi zilizoonekana na shirika la habari la AP, Blaise Compaore anashtumiwa kwa makosa ya kushiriki mauaji, kuhujumu usalama wa taifa na kuficha maiti. Compaore ambae anaishi uhamishoni nchini Ivory Coast tangu alipoondolewa madarakani mwaka 2014, atahukumiwa akiwa hayupo mahakamani. Ivory Coast imekua ikikataa kumrejesha Compaore nchini mwake licha ya Burkina Faso kutoa waranti wa kukamatwa kwake miaka sita iliyopita.

Familia yataka kesi ya kweli na wazi

Mariam Sankara, mjane wa Thomas SankaraPicha: Getty Images/AFP/A. Ouoba

Mshirika mkuu wa zamani wa Compaore Generali Gilbert Diendere ni miongoni mwa watuhumiwa katika kesi hiyo ambayo inatarajiwa kudumu miezi kadhaa na inayotajwa kuwa muhimu ili kufahamu mazingira yaliyogubika kifo cha Sankara, yaliyofichwa kwa takriban miaka 35.

Prosper Farama mmoja wa mawakili wa wahasiriwa, alisema kuwa wanachotarajia katika kesi hii ni ukweli na kupatikana haki kwa sababu kwa sasa, kuna maelezo yanayokinzana kuhusu kilichotokea wakati wa kifo cha Sankara. Nae Mariam Sankara, mjane wa kiongozi huyo, alipowasili mahakamani alisema huu ni wakati waliokua wakiusubiri na kwamba kesi hiyo ni muhimu ili mazoea ya kutowawajibisha wahalifu barani Afrika yakomeshwe.

Kwa upande wao, mawakili wa Compaore wameelezea kuwa Rais huyo wa zamani hatohudhuria wala kushiriki kesi hiyo kwa kuwa hakuwahi kuitwa ili kuhojiwa kabla ya kushtakiwa.

Sankara shujaa wa Afrika ?

Picha: picture-alliance/dpa/Tanjug

Sankara, kiongozi mcheshi na aliyetajwa kuwa "Che Guevara wa Afrika", amekuwa na ushawishi mkubwa katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika aliyoibadili jina kutoka lile la ukoloni wa Ufaransa la "Upper Volta" hadi Burkina Faso ambayo inamaanisha "Ardhi ya wanaume waaminifu" katika lugha zinazozungumzwa nchini humo za Moore na Dioula.

Sankara aliingia madarakani mwaka 1983 akiwa na umri wa miaka 33 baada ya yeye na Compaore kulipindua jeshi lenye msimamo wa wastani. Utawala wa Sankara ulijikita zaidi katika ajenda za ujamaa na serikali yake ilipinga ukeketaji, ndoa za wake wengi na hata zile za kulazimishwa.

Sankara amebaki kuwa kipenzi cha wengi na mwenye kuheshimiwa barani Afrika kutokana na kuzipinga mamlaka za kimagharibi.Lakini mnamo mwaka 1987 Compaore alimsaliti rafiki yake kwa kumpindua madarakani na kuchukua madaraka ya nchi hiyo ambayo aliiongoza kwa miaka 27 kwa mkono wa chuma kabla ya kuondolewa pia madarakani kufuatia maandamano ya umma. Washirika wake wa karibu wanamkumbuka kama kiongozi aliyejitolea na mwenye umakini wa hali ya juu.

Tishio la ugaidi kwenye kanda ya sahel

Kesi hii inasikilizwa katika wakati ambapo Burkina Faso inakabiliwa na ongezeko la vurugu zinazohusishwa na Al Qaida na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, makundi ambayo yameua maelfu ya watu na kusababisha watu wengine zaidi ya milioni 1.4 kuyahama makaazi yao na kupelekea mgawanyiko katika nchi ambayo ilijulikana kwa jamii ya Wakristo na Waislamu kustahamiliana na kuishi kwa amani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW