Kesi ya Oscar Pistorius yasikilizwa June 4
31 Mei 2013Kisa cha Oscar Pistorius kinaingia awamu ya pili:mwanariadha mlemavu wa Afrika kusini anaetuhumiwa kuhusika na mauwaji atafikishwa mahakamani Juni nne ijayo.Mwanariadha huyo alituhumiwa miezi kama mitatu hivi iliyopita,tena mnamo "siku ya wapendanao",kumpiga risasi na kumuuwa mpenzi wake Reeva Steenkamp,Baada ya siku nane rumande,aliachiwa huru kwa dhamana.Kesi iliakhirishwa hadi Juni.
Ilikuwa usiku wa februari 13 kuamkia 14:Oscar Pistorius alimpiga risasi mpenzi wake Reeva Steenkamp katika jumba lake la fakhari katika kitongoji cha Pretoria.Mwendesha mashtaka anamtuhumu kuhusika na mauwaji..Mwenyewe Pistorius anasema alidhani wameingiliwa na mwizi.Kesi kwa hivyo itaanza kusikilizwa jumanne,juni nne ijayo.
Medupe Simasiku,msemaji wa ofisi ya mwendesha mashtaka katika jiji la Pretoria anaelezea kile anachotuhumiwa kufanya:"Anatuhumiwa kuundaa mauwaji,hakuna mashtaka mengine."
Kaua au anasingiziwa?
Kisa cha mwanariadha Oscar Pistorius hakiwazungushi kichwa wananchi wa Afrika kusini peke yao,vyombo vya habari vya ulimwengu mzima vimeingia mbioni.Iliripotiwa vya kutosha kuhusu "kuporomoka" vibaya sana "mwendaji mbio anaetumia miguu ya chuma."Jina hilo la utani alipewa msimu wa kiangazi mwaka 2012,kwasababu alikuwa mwendaji mbio wa kwanza aliyekatwa miguu yoyote miwili,ambae ameshiriki katika michezo ya Olympik akiwa na miguu ya kubandika.Alifanikiwa sio tu kuingia nusu fainali ya mbio za mita 400,bali pia fainali ya mbio za mita 400 kupokezana mara nne.Alishiriki pia katika michezo ya olympik ya walemavu na kufanikiwa kurejea nyumbani na medali mbili za dhahabu na moja ya fedha.Nyumbani alipokelewa kwa shangwe,anasimulia Janet Whitton,ambae ni ripota wa michezo katika kituo cha televisheni cha SABC 1 cha Afrika kusini."Wote walimpenda.Bila ya kujali wanatoka kataika kabila gani au tabaka gani ya jamii.Na hata wale ambao hawakuwa wakivutiwa na michezo,aliwavutia."Anasema Janet Whitton.
Ndio maana mshituko ulikuwa mkubwa kupita kiasi.Wapita njia waliozungumza na DW siku ya pili baada ya Steenkamp kuuliwa nchini Afrika kusini walikuwa na maoni tofauti.Kuna waliosema wanamuamini.Wengine wanasema walihitaji muda kwanza kuweza kutathmini yaliyotokea.Wengine wamepigwa na bumbuwazi na kuna wengine wanaosema ilikuwa ajali tu,hawaamini kama Oscar Pistorius anaweza kumuuwa mtu kama vile.
Hivi sasa,miezi mitatu baada ya kisa hicho kutokea,waafrika kusini wamezidi kuingiwa na hofu.Wanajiuliza kama kweli hana hatia.Janet Whitton :"Nchini Afrika kusini idadi ya visa vya uhalifu ni kubwa mno,kuna matumizi ya nguvu dhidi ya akinamama na ndio maana hakuna anaemuonea huruma.Tangu Reeva Steenkamp alipouliwa,mengi yanayomhusu Pistorius yamefichuliwa pia.Ghadhabu zake,jinsi anavyovutiwa na silaha na meengineyo ambayo hayatoi picha nzuri."
Kesi itaakhirishwa tena
Kiu cha walimwengu kutaka kujua mengi zaidi kumhusu Pistorius kimepungua kidogo
Korti ya mjini Pretoria imeshasema kesi hiyo itasikilizwa kwa dakika kumi tu na baadae kuakhirishwa hadi mwezi Agosti.Hukmu haijulikani itatolewa lini.
Mwandishi:Schwarzbeck,Nadina/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed