1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya rufaa ya chama cha AfD yaanza Ujerumani

12 Machi 2024

Mahakama moja ya nchini Ujerumani imeanza kusikiliza kesi ya rufaa inayohusu kuorodheshwa kwa Chama Mbadala kwa Ujerumani AfD kama kundi linaloshukiwa kuwa la itikadi kali

Deutschland, München, Bayern | Eine Afd Fahne wird auf einer Kundgebung hochgehalten
Picha: Sachelle Babbar/picture alliance/ZUMAPRESS

Siku ya Jumanne, jaji anayesimamia kesi hiyo Gerald Buck alikataa ombi la chama hicho cha AfD la muda zaidi wa kupitia na kuelewa ushahidi wa maelfu ya kurasa dhidi yake, hali iliyomfanya wakili wa chama hicho Christian Conrad kuomba kubadilishwa kwa jopo zima la majaji waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo.

Wakili wa AfD asema majaji wana upendeleo

Conrad amesema kuwa chama cha AfD kisichopenda wageni kinataka kubadilishwa kwa jopo hilo zima la majaji akitoa hoja kuwa majaji hao wana upendeleo.

Soma pia:Umaarufu wa AfD wapungua kufuatia maandamano Ujerumani

Wakili huyo ameeleza kuwa hatua ya mahakama hiyo ya mjini Muenster kukataa kuongeza muda kabla ya kusikizwa kwa kesi hiyo ni ishara wazi ya upendeleo. Buck alikataa ombi hilo na kulitaja kama ukiukaji wa haki ya mlalamishi.

AfD yajipata chini ya shinikizo kutokana na vitendo vya viongozi wake

Chama hicho kinachoegemea siasa kali za mrengo wa kulia kimekabiliwa na shinikizo kubwa baada ya hivi karibuni kutolewa ripoti kwamba viongozi wake wakuu walihudhuria mkutano na kundi la watu wanaopigania sera za kuwafukuza watu wote wasiokuwa na asili ya Ujerumani.

Soma pia:Ujerumani yakumbwa na maandamano ya kupinga itikadi kali za mrengo wa kulia

Ikiwa uamuzi wa kesi hiyo utabainisha kuwa idara ya upelelezi wa ndani nchini Ujerumani, BfV ilikuwa sahihi katika kukiorodhesha chama hicho cha AfDna tawi lake la vijana kama washukiwa wa itikadi kali, idara ya usalama itaruhusiwa kutumia mbinu zote za kijasusi dhidi ya chama hicho ikiwemo udukuzi wa mawasiliano ya simu na kukusanya habari kukihusu.

Raia wa Ujerumani waandamana dhidi ya chama cha AFD Picha: Sebastian Kahnert/dpa/picture alliance

Uamuzi kama huo utakuwa pigo kubwa kwa chama hicho ikiwa imesalia takriban miezi sita kabla ya uchaguzi wa majimbo na ule wa bunge la Ulaya.

Mahakama ya chini ya mjini Cologne, inakopatikana idara hiyo ya ujasusi, ilithibitisha tathmini hiyo ya BfV mnamo mwaka 2022 na kuruhusu ofisi hiyo kufuatilia chama hicho kama mshukiwa.

Mahakama ya juu ya jimbo la North Rhine-Westphalia sasa itaamua iwapo tathmini ya awali ilikuwa halali.

Soma pia:Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Ujerumani AfD chasema EU ni mradi ulioshindwa

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, zaidi ya watu 100 wanaofanya kazi ndani ya chama hicho AFD ama wabunge wa chama hicho, wanatajwa kama sehemu ya mashirika ambayo yameorodheshwa kama yanayoegemea itikadi kali za mrengo mkali wa kulia.

AfD yapinga ripoti ya vyombo vya habari

Ripoti iliyochapishwa leo na shirika la habari la Bayerischer Rundfunk (BR) ambalo lilitegemea orodha ya majina ya ndani ya bunge la Ujerumani na kitabu cha kumbukumbu ya majina ya wafanyikazi kutoka kundi la wabunge wa AfD, imesema kuwa wafanyakazi hao wanajumuisha watu waliotajwa katika ripoti za idara za ujasusi wanaoshikiia nafasi za uongozi katika mashirika yanayofuatiliwa na idara hizo ambao wamejitokeza kama wazungumzaji katika Taasisi ya Sera za Serikali IFS katika mji wa Mashariki wa Schnellroda inayoorodheshwa kama inayoegemea itikadi kali za mrengo mkali wa kulia.

Kundi la wabunge waAfD limepinga vikali ripoti hiyo.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW