Kesi ya rushwa dhidi ya kampuni ya Shell na Eni yaanza
14 Mei 2018Mashitaka hayo yanalengo la kutaka leseni za makampuni hayo zifutwe.
Mji wa Milan nchini Italia kuanzia leo utakuwa sehemu ya jukwaa la mwezi mzima litakalojishughulisha na kuweka wazi biashara chafu katika sekta ya mafuta. Mwendesha mashtaka wa mji wa Milan nchini Italia anataka kuyawajibisha makumpuni ya Eni la Italia pamoja na Shell la Uingereza, kwa kutoa hongo ya mamilioni ya fedha ili kupata leseni ya kufanyakazi nchini Nigeria.
Watu 15 wanashitakiwa, wengi wao wakiwa wafanyakazi wa makampuni hayo mawili , kwa kuhusika na rushwa.
Sio tu katika mji wa Milan ambako makampuni hayo yatakabiliwa na kesi, lakini pia mjini Lagos kutakuwa na kesi nyingine dhidi ya makamuni hayo makubwa ya mafuta.
Katika kesi hiyo mjini Lagos makampuni hayo yatakabiliwa na kesi iliyofikishwa mahakamani na makundi ya haki za binadamu HEDA, Human and Environmental Development Agenda, ajenda kwa ajili ya maendeleo ya watu na mazingira dhidi ya makampuni hayo. HEDA inataka kampuni ya Shell na Eni ifutiwe leseni zao. Kesi hizo zote zinahusu matukio yaliyotokea mwaka 2011.
Rushwa na ubadhirifu
Wakati huo kampuni za Shell na Eni zililipa kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.3 katika akaunti ya serikali ya Nigeria. Kwa kiwango hiki cha fedha makampuni hayo yalitaka kupata uhakika wa kumiliki kitalu cha mafuta namba OPL 245 , kitalu ambacho kwa maelezo ya makampuni hayo kinaweza kutoa mafuta yenye thamani ya hadi dola bilioni 3. Kiasi kikubwa cha fedha hizo kilitumbukia sio katika hazina ya serikali ya Nigeria , badala yake zilikwenda katika kampuni ya Maluba inayojishughulisha na mafuta na gesi.
Serikali ya Nigeria tayari imekwisha jieleza katika kesi iliyofanyika nchini Uingereza , kwamba ununuzi wa leseni hiyo kwa ajili ya eneo hilo kubwa la mafuta mwaka 2011 ni kinyume na sheria, amesema msemaji wa kundi la HEDA Lanre Suraju katika mahojiano na DW. Kutokana na fedha hizo za ununuzi dola milioni 520 zilikuwa taslimu na kwamba ni fedjha za rushwa zilizogawanywa kwa wanasiasa.
Serikali hata hivyo iliambulia kiasi cha dola milioni 210 tu. Mhusika mkuu katika kampuni ya Malabu Oil & Gas ni Dan Etete , ambaye katika miaka ya 1990 alifanyakazi chini ya utawala wa dikteta Sani Abacha kama waziri wa mafuta.
Katika wadhifa huo aliwahi mwaka 1998 kupata leseni ya kuchimba mafuta na kuihamishia katika kampuni yake. Etete alihukumiwa mwaka 2007 nchini Ufaransa kwa kufanya biashara haramu ya fedha . Alipaswa pia kufikishwa mahakamani mjini Milan, lakini kwa mujibu wa Lanre Surahu , Etete kwa sasa hajulikani aliko.
Mwandishi: Martina Schwikowski /ZR/ Sekione Kitojo
Mhariri: Iddi Ssessanga