1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya shambulizi la Charlie Hebdo yaanza kusikilizwa

Daniel Gakuba
2 Septemba 2020

Kesi ya watu wanaotuhumiwa kufanya mashambulizi dhidi ya waandishi wa gazeti la vibonzo la Charlie Hebdo na duka la Wayahudi vyote vya mjini Paris, Ufaransa imeanza kusikilizwa siku ya Jumatano.

Frankreich Paris Laurent "Riss" Sourisseau | Charlie Hebdo
Picha: pictur- alliance/dpa/Maxppp/O. Lejeune

Kesi hiyo inajumuisha watuhumiwa 14, wanaume watatu na mwanamke mmoja, lakini waliokuwa kizimbani siku ya Jumatano mjini Paris ni wanaume 11. Mwanamke pekee katika kesi hiyo pamoja na wanaume wawili wanashtakiwa bila kuwepo, kwa sababu waliondoka kujiunga na kundi la IS.

Wote wanatuhumiwa kununua magari, silaha na vifaa vingine vilivyotumiwa katika mashambulizi hayo yaliyofanyika Januari mwaka 2015.

Wengi wa wale waliokuwepo mahakamani, wamejitetea wakisema walipokuwa wakinunua vifaa hivyo, walidhani vitatumiwa katika uhalifu wa kawaida. Hata hivyo Patrick Klugman, mmoja wa mawakili wa wahanga wa mashambulizi, amesema anayemsaidia mhalifu, yeye pia ni mhalifu.

''Wale walioko hapa, hawako tu hivi hivi, kuna sababu. Kosa lao sio dogo, hakuna kosa la ugaidi lililo dogo. Bila ya wao, hakungekuwa muuaji, kwa sababu asingepata silaha, fedha, wala kujua pa kwenda. Tafadhali, wao sio wasaidizi tu katika uhalifu.''

Mawakili wakiwasili mahakamani mjini ParisPicha: picture-alliance/abaca/B. Eliot

Kesi hiyo imefanyika chini ya ulinzi mkali, huku watu wote waliotaka kuingia katika chumba cha mahakama wakilazimika kupitia katika vituo kadhaa vya ukaguzi wa maafisa wa usalama.

Mlolongo wa mashambulizi wa kundi la IS ya mwaka 2015 ulianza na lile kwenye ofisi za gazeti la vibonzo la Charlie Hebdo, ambapo washambuliaji watatu wenye bunduki waliwauwa kwa risasi watu 17, na kisha wao pia wakauawa.

Baadaye, genge la wanamgambo wa IS nchini Ubelgiji liliwauwa watu 130 katika ukumbi wa dansi wa Bataclan, uwanja wa taifa wa soka mjini Paris na katika baa na mikahawa. Soma Washambuliaji wa Charlie Hebdo watafutwa

Gazeti la Charlie Hebdo lililengwa kutokana na kuchapisha katuni ya Mtume Mohammad miaka kadhaa kabla ya shambulizi hilo.

Watu wengi duniani walionyesha mshikamano wa mji wa Paris wakati wa mashambulizi hayo, lakini pia zimekuwepo shutuma kwa vyombo vya usalama vya mji huo, kwamba washambuliaji walifanikiwa katika hila zao kutokana na uzembe wa vyombo hivyo.

Kwenye mkesha wa kusikilizwa kesi hii, gazeti la Charlie Hebdo limechapisha tena katuni ya Mtume Mohammad iliyoliletea matatizo, hatua iliyolaaniwa na chuo kikuu cha kiislamu cha al-Azhar cha nchini Misri, kilichoilinganisha na kauli ya chuki, ambayo ni tusi kwa waumini waadilifu wa dini ya Kiislamu.

(ape,dpae, afpe)

 

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW