1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Trump kuanza leo wakati mawakili wake wakikosoa

Sylvia Mwehozi
9 Februari 2021

Baraza la seneti la Marekani leo litaanza mchakato wa kusikiliza kesi inayomkabili rais wa zamani Donald Trump, wakati timu ya mawakili wa kiongozi huyo ikidai kwamba mashitaka dhidi yake ni kinyume na katiba

USA Ex-Präsident Donald Trump Rede
Picha: Luis M. Alvarez/AP Photo/picture alliance

Trump anakabiliwa na tuhuma za uchochezi wa ghasia zilizotokea Januari 6 katika uvamizi wa majengo ya bunge, shambulio ambalo lilishangaza taifa na ulimwengu ujumla. Rais huyo wa zamani wa Marekani anatuhumiwa kuhimiza wafuasi wake kuvamia bunge wakijaribu kuingilia kati mchakato wa kuidhinisha ushindi wa rais mteule wakati huo Joe Biden.

Hakuna mashahidi wanaotarajiwa kuitwa kwenye kesi hiyo kwasababu maseneta ambao wameapishwa kuwa wazee wa baraza watatumia vidio za tukio zima waliloshuhudia na kulazimika kukimbia kwa ajili ya usalama. Trump mwenyewe amekataa wito wa kutoa ushahidi. Anakuwa rais wa kwanza kukabiliwa na mashitaka baada ya kuondoka madarakani na wa kwanza kushitakiwa mara mbili.

Timu ya mawakili wanaomtetea rais huyo wa zamani, wametoa mashambulizi dhidi ya kesi hiyo wakisema "ni ukumbi wa michezo ya kisiasa". Wanadai kuwa mashitaka hayo ni kinyume na katiba na kusema ni "upuuzi" kwa kujaribu kumwajibisha rais wa zamani kwa uasi wa Januari.

Wafuasi wa Trump waliovamia bungePicha: Douglas Christian/Zumapress/picture alliance

Timu hiyo inapanga kuwasilisha hoja juu ya uhalali wa kesi yenyewe na vilevile kitendo cha kumtwisha lawama kiongozi huyo kwa ajili ya uasi uliotokea. Wanapendekeza kwamba Trump alikuwa akitumia haki yake ya kikatiba pale alipowahimiza wafuasi wake kuandamana kwenye majengo ya bunge, na kwamba baraza la Seneti halina mamlaka ya kumshitaki Trump mara baada ya kuondoka madarakani.

Chini ya makubaliano baina ya kiongozi wa wengi katika Seneti Chuck Schumer na kiongozi wa Republican Mitch McConnell, hoja za ufunguzi zitaanza kesho Jumatano mchana, kwa kila upande kuwasilisha hoja zake kwa saa 16. Mitch McConnell anaongeza kuwa; 

"Muundo huu umekubaliwa na timu ya wanasheria wa rais wa zamani Trump na baraza la wawakilishi kwasababu ni utaratibu mzuri na unatoa haki za pande zote mbili. Itawapa muda wa kutosha maseneta kama mahakimu kupitia kesi hiyo na hoja ambazo kila upande utawasilisha".

Upande wa baraza la wawakilishi nao umewasilisha nyaraka zake ukisisitiza kwamba Trump "aliwasaliti Wamarekani" na hivyo hakuna hoja ya msingi ya kukwepa hilo au utetezi. "Uchochezi wake wa uasi dhidi ya serikali ya Marekani, ambao uliingilia mchakato wa amani wa kukabidhiana madaraka, ni moja ya uhalifu mkubwa wa kikatiba ambao uliwahi kutendwa na rais", imesema taarifa ya upande wa Democrats.

Kesi hiyo itaanza Jumanne kwa mjadala na kisha kufuatiwa na kura ya iwapo inaruhusiwa kikatiba kumshitaki rais wa zamani, hoja ambayo inaweza kuwashughulisha Republican wanaotamani kumwokoa Trump.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW