1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya ugaidi dhidi ya Rusesabagina yaanza mjini Kigali

Daniel Gakuba
17 Februari 2021

Mahakama ya Rwanda imeanza leo kusikiliza kesi dhidi ya meneja wa zamani wa hoteli ya Mille Collines mjini Kigali, Paul Rusesabagina, ambaye alipata umaarufu kimataifa kupitia filamu ya Hollywood, Hotel Rwanda.

Ruanda Kigali | Paul Rusesabagina wird zu Gericht eskortiert
Picha: Clement Uwiringiyimana/Reuters

Rusesabagina anakabiliwa na mashtaka 13, yakiwemo ya ugaidi na kuongoza kundi la waasi wenye silaha. Kesi hiyo pia inawahusisha watuhumiwa wengine wapatao 20. Wanahusishwa na kundi lijulikanalo kama FLN (Force de Liberation National) ambalo mwaka 2018 lilidai kufanya mashambulizi kusini mwa Rwanda, ambapo watu kadhaa waliuawa na mali kuharibiwa.

Kulingana na shirika la habari la Reuters, amekiri kulisaidia kifedha kundi hilo, ila akakanusha kufanya kosa lolote.

Soma zaidi: 'Shujaa wa Hotel Rwanda' kukabiliwa na miaka 25 jela

Akizungumza mahakamani leo, Rusesabagina amesema mahakama ya Rwanda haina uwezo kisheria wa kuendesha kesi dhidi yake, kwa hoja kwamba yeye ni raia wa Ubelgiji aliyefikishwa nchini Rwanda kinyume na sheria za kimataifa.

Katika filamu ya Hotel Rwanda, Don Cheadle alicheza nafasi ya Paul RusesabaginaPicha: picture-alliance/dpa/Tobis Film

Kesi hii inafuatiliwa kwa karibu na jumuiya ya kimataifa, na tayari Marekani na Umoja wa Ulaya zimeiwekea shinikizo Rwanda ihakikishe kesi hiyo inaendeshwa kwa uwazi.

Shujaa wa filamu ya 'Hotel Rwanda'

Filamu hiyo ya Hotel Rwanda iliumulika mchango wa Paul Rusesabagina katika kuwaokoa watu zaidi ya 1200 waliokuwa wakiindwa ili wauwawe katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Aliondoka nchini Rwanda mwaka 1996 na kupata uraia wa Ubelgiji mwaka 2000, na anayo hadhi ya kudumu ya kuishi nchini Marekani. Tarehe 31 Agosti, 2020 alionyeshwa na ofisi ya mwendesha mashtaka mjini Kigali katika hali ya kushtukiza, na hadi leo haijawa bayana namna alivyosafirishwa hadi Rwanda. Familia yake inadai alitekwa nyara mjini Dubai.

Soma zaidi: Mawakili wahofia huenda Paul Rusesabagina akateswa Rwanda

Rusesabagina amekuwa mpinzani mkubwa wa rais wa sasa wa Rwanda, Paul Kagame tangu mwaka 2005, akiongoza chama cha upinzani kilichofanya kazi uhamishoni. Mwaka huo huo alitunukiwa tuzo muhimu ya Marekani na Rais wa wakati huo George W. Bush, ambayo imetolewa pia kwa watu maarufu kama Mama Teresa wa Calcuta.

Mpinzani wa serikali ya Rais Paul Kagame

Serikali ya mjini Kigali inamchukulia kama adui ambaye amejijengea umaarufu kupitia hila za uongo, na kukanusha simulizi za ushujaa wake wa kuwaokoa mamia ya Watutsi waliokuwa wakiwindwa.

Paul Kagame, Rais wa RwandaPicha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

Baadhi ya watu walionusurika katika hoteli yake pia wamekuwa wakiunga mkono mtazamo huo wa serikali.

Wakati filamu ya Hotel Rwanda ilipoonyeshwa kwa mara ya kwanza katika uwanja wa mpira mjini Kigali mwaka 2005, bwana Rusesabagina alitarajiwa kuhudhuria lakini hakuwasili, na wakati huo ilielezwa kuwa alikuwa ameugua ghafla.

Soma zaidi: Rais Kagame ajitokeza na kukomesha uvumi kuhusu kifo chake

Baadaye ilifahamika kuwa alikuwa ametoa kauli za kuikosoa serikali ya Rwanda, na hadi alipoonyeshwa kwa vyombo vya habari akifungwa pingu Agosti mwaka jana, alikuwa hajakanyaga tena kwenye ardhi ya Rwanda.

 

Vyanzo: dpae, rtre

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW