1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliokamatwa ni pamoja na Raia wa Ujerumani, Peter Teudtner

Amina Abubakar 25 Oktoba 2017

Wanaharakati 11 wa haki za binaadamu akiwamo mkuu wa shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International Uturuki Idil Eser  wamefikishwa mahakamani nchini Uturuki kwa madai ya kusaidia makundi ya kigaidi.

Amnesty International Protest Türkei Festnahmen
Nembo ya Shirika la Amnesty ikiwa katika mikono yenye pingu, alama inayoonyesha kuwa shirika hilo linazuiwa kufanya kazi yake. Picha: Getty Images/E.Dunand

Watu hao wameshtakiwa kwa makosa ya Ugaidi  kesi inayotarajiwa kusababisha tofauti kubwa kati ya uturuki na washirika wake wa Ulaya. Polisi ilizingira eneo la kuingilia mahakamani  lakini waandishi habari na wafuasi  walioshtakiwa walikusanyika katika eneo hilo.

Kundi la takriban watu 50 kutoka makundi ya kutetea haki za binaadamu, mabalozi wa kigeni na makundi ya kutetea haki za wanawake walisimama nje ya mahakama wakibeba mabango yaliyoandikwa waachie "watetezi wa haki za binaadamu”

Aidha wanaharakati waliofikishwa mahakamani ni pamoja na  raia wa Ujerumani Peter Teudtner, raia wa Sweden Ali Gharavi  na raia wa Uturuki Idil Eser na huenda wakahukumiwa miaka 15 jela ikiwa watakutwa na hatia, katika  mashitaka yanayojumuisha kujiunga na makundi ya kigaidi pamoja na kuyasaidia makundi hayo ya kigaidi yaliyojihami. 

Watetezi wa haki za binaadamu nje ya jengo la mahakama mjini InstanbulPicha: Reuters/O.Orsal

Washtakiwa walikamatwa kwa mara ya kwanza mwezi Julai baada ya kuhudhuria warsha juu ya usalama wa teknolojia iliyoandaliwa katika kisiwa kimoja karibu na mji wa  Istanbul.

Taasisi kadhaa za kutetea haki za binaadamu zimeendelea kukemea hatua ya kushikiliwa kwa baadhi ya watetezi. 

Aidha kesi hiyo imezidi kuongeza wasiwasi kwamba Uturuki ambayo ni mwanachama wa Umoja wa kujihami NATO aliye karibu na eneo la mizozo ya Iraq, Iran na Syria inatumbukia katika utawala wa kidikteta chini ya rais Tayyip Erdogan.

Erdogan asema kamata kamata itadumisha uthabiti wa Uturuki

Hata hivyo Rais Erdogan anasema kamata kamata ya watu zaidi ya 50,000 inayofanywa tangu kufanyika mapinduzi yaliyoshindwa mwaka uliopita ni muhimu katika kudumisha uthabiti wa nchi yake. Wengi wa waliokamatwa bado wanasubiri kufikishwa mahakamani.

"Ni dhahiri hii ni kesi ya watetezi wa haki za binaadamu waliohudhuria Warsha katika kisiwa mjini Istanbul, lakini kwa sasa ni mfumo wa haki uturuki na serikali ya nchi hiyo wanaojihukumu," alisema John Dalhuisen, Mkurugenzi wa shirika la Amnesty Ulaya na Asia ya kati alipokuwa nje ya mahakama hiyo. 

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan Picha: picture-alliance/AA/Turkish Presidency/Handout/Y. Bulbul

Aidha mwenyekiti wa shirika la  Amnesty Uturuki  Taner Kilic, alikamatwa na kufungwa mapema mwaka huu kwa kesi tofauti  lakini baadaye alijumuishwa katika madai kama ya washtakiwa wa leo ya kuhusika na masuala ya kigaidi.

Uamuzi wa leo umeyaweka mahusiano ya Uturuki na Umoja wa Ulaya mahala pabaya wakati nchi hiyo ikiwa na nia ya kujiunga na Umoja huo.

Muda mfupi baada ya kamata kamata Ujerumani ilisema inaangalia upya ombi la Uturuki la kununua silaha kutoka kwake, huku Kansela Angela Merkel akisema jaribio la miaka 12 la Uturuki kujiunga na Umoja huo linahitaji kusimamishwa. Hata hivyo Uturuki imesema bado itaendelea kusukuma ajenda yake hiyo.

Mwandishi: Amina AbubakarAFP/dpa

Mhariri: Gakuba, Daniel