1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya watuhumiwa wa siasa kali ya mrengo wa kulia

16 Aprili 2013

Kuakhirishwa kesi ya watuhumiwa wa siasa kali ya mrengo wa kulia,maridhiano kuhusu kutengwa idadi maalum ya nyadhifa za juu kwaajili ya wakinamama na Venezuela ni miongoni mwa mada magazetini .

)
Maandamano ya Munich dhidi ya chama cha siasa kali za mrengo wa kuliaPicha: Getty

Tuanzie Munich na mada iliyozusha mlalamiko ndani na nje ya Ujerumani kuhusu kesi ya watuhumiwa wa mauwaji ya watu 10 katika jiji la Cologne ambao wanane kati yao walikuwa waturuki.Kesi hiyo ambayo maandalizi yake yamegubikwa na ila za kila aina na ambayo ilikuwa ifunguliwe kesho,imeakhirishwa hadi May sita ijao.Gazeti la Rhein-Necker Zeitung la mjini Heidelberg linaandika:

Kwanza kesi hiyo haijaruhusiwa kusikilizwa katika ukumbi mkubwa au kupatikana njia ya kutangazwa katika ukumbi mwengine kwa msaada wa video.Baadae ukafuata utaratibu usioeleweka ambapo hata mwaandishi habari mmoja wa kituruki hakuruhusiwa kusikiliza kesi hiyo ingawa wanane kati ya wahanga kumi wa mauwaji ni waturuki.Hata shauri la waandishi habari wa kijerumani kuwaachia nafasi zao wenzao wa kituruki lilikataliwa.Hatimae sasa utaratibu mzima unaanza upya.Mashahidi takriban 370 wataitwa,hata ratiba imevurugika.Yote hayo kwanini?Jibu ni kwamba mahakama ya juu ya mjini Munich imedhamiria kuhakikisha kila kitu kinafanyika ipasavyo.

Uamuzi wa maana

Gazeti la "Pforzheimer Zeitung"linatathmini uamuzi wa kuakhrishwa kesi hiyo kama ifuatavyo:

Kwa kuakhirisha kusikilizwa kesi hiyo mahakama imetaka kutoa ishara;wameelewa na wamedhamiria kila kitu kifanyike kama inavyostahiki.Wiki tatu zinahitajika kuleta uwazi katika maandalizi,kupunguza shinikizo la vyombo vya habari na hatimae kuhakikisha kesi inafanyika kwa utulivu .

Vidonge vinamezeka?

Waziri wa ajira Ursula von der Leyen,mmojawapo wa wanaopigania viwango maalum vya idadi ya wakinamama katika tabaka za uongoziPicha: Clemens Bilan/dapd

"Ursula von der Leyen amezicheza karata na kushinda:" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la mjini Cologne,Kölner Stadt Anzeiger kuhusu mvutano ndani ya chama cha Christian Democratic Union CDU kati ya wanaodai na wanaopinga paweko idadi maalum ya wakala wa wakinamama katika mashirika makubwa makubwa ya humu nchini.Hata hivyo gazeti la "Dresdner Neueste Nachrichten" linahisi:

Ilikuwa kama biashara ya ng'ombe:Uongozi wa CDU unataka kuwatuliza wanaopendelea pawepo idadi maalum ya wakinamama katika uongozi.Kana kwamba kiwango kidogo ni sawa na balaa linaloweza kuikumba serikali ya muungano wa vyama vya CDU/CSU na waliberali wa FDP.Azma ya kuanzisha sheria ya kutengwa idadi maalum ya vyeo kwaajili ya akinamama kuanzia mwaka 2020, kijuu juu inaonekana kana kwamba viongozi wa CDU/CSU/FDP wametaka kuwaridhia akina Ursula von der Leyen na wenzake.Ni ahadi isiyo thabiti na ambayo hakuna ajuaye kama itatekelezwa.Kwa hivyo hakuna ajuaye kama wakosoaji watakubali kuvimeza vidonge hivyo.Vyama ndugu vya CDU/CSU hapo vinatilia maanani zaidi msimamo wa chama kidogo cha FDP katika kuwaridhisha wapiga kura wake kuliko msimamo wao wenyewe.

Mustakbal wa Venezuela baada ya Chavez

Rais mpya wa Venezuela Nicolas MaduroPicha: LUIS ACOSTA/AFP/Getty Images

Na mada yetu ya mwisho inamulika uchaguzi wa rais nchini Venezuela uliompatia ushindi Nicolas Maduro.Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linaandika:

Si kazi rahisi inayomsubiri rais mpya wa Venezuela.Hakuna anaebisha kwamba Hugo Chaves amewatoa wananchi wengi katika hali ya maskini.Lakini juhudi hizo zimesababisha mtengano nchini.Matokeo ya uchaguzi wa rais yamethibitisha jinsi nchi ilivyogawika.Na matatizo hayatopungua.Matumizi ya nguvu yaliyokithiri,ughali wa maisha,mashirika ya umma yanayokurubia kufilisika na uhaba wa huduma na mahitaji ya jamii,yote hayo yanawafanya wananchi wazidi kulalamika.Maduro atabidi kufuata njia nyengine kinyume na ile ya mtangulizi wake Chavez.Akitaka kulinda madaraka yake,hatokuwa na budi isipokuwa kusaka ushirikiano na upande wa upinzani ili kurejesha suluhu ya taifa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi