1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Kevin McCarthy aondolewa kama Spika wa Bunge la Marekani

Saleh Mwanamilongo
4 Oktoba 2023

Mchakato wa kumwondoa McCarthy, ulianzishwa na wabunge wa chama cha Republican waliokasirishwa na uamuzi wake wa kushirikiana na chama cha Democratic.

Kevin McCarthy ametimuliwa katika uasi wa mrengo wa kulia wa chama cha Republican
Kevin McCarthy ametimuliwa katika uasi wa mrengo wa kulia wa chama cha Republican Picha: J. Scott Applewhite/AP/picture alliance

Kevin McCarthy ametimuliwa katika kile kilichoelezewa na wabunge wa Republican kuwa ushirikiano wake na wanachama wa chama cha Democratic. Kevin McCarthy amefukuzwa katika uasi wa mrengo wa kulia mara ya kwanza kabisa kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani kupoteza kura ya kutokuwa na imani naye. Matokeo ya mwisho yalikuwa 216 dhidi ya 210 kumng'oa mbunge wa California kama kiongozi wa walio wengi wa chama cha Republican katika baraza la Congress.

Wanachama wanane pekee wa Republican walipiga kura ya kumuondoa Kevin McCarthy katika kura hiyo ya Jumanne. Aliweza kupata uungwaji mkono kutoka kwa wabunge 210 - wote wa Republican. Lakini Democrats waliungana na waasi wa Republican kumwangusha Spika.

''Machafuko ni Spika McCarthy''

Mbunge wa Republican Matt Gaetz ambaye alianzisha vuguvugu la kumtimua Spika Kevin McCarthy amesema walikuwa wamepoteza imani naye.

''Mheshimiwa Spika, rafiki yangu wa Oklahoma anasema mimi na wenzangu ambao hatumuungi mkono Kevin McCarthy tutaingiza Bunge na nchi katika machafuko. Machafuko ni Spika McCarthy. Machafuko ni mtu ambaye hatuwezi kumwamini kwa maneno yake.'', alisema Gaetz.

Aliendelea kusema : ''Jambo ambalo Ikulu, chama cha Democratic, na wengi wetu katika upande wa kihafidhina wa Republican tungebishana ni kwamba jambo ambalo limetuweka pamoja ni Kevin McCarthy kusema kitu kwetu sote wakati mmoja au mwingine ambacho hakufanya."

Mpasuko wa chama cha Republican ?

Hakuna mrithi dhahiri wa kusimamia wabunge Republican walio wengiPicha: Jon Cherry/REUTERS

Kabla ya kura hiyo Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump alichapisha kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, kwamba chama hicho kinapaswa kupigana na Wademocrat wenye msimamo mkali badala ya wao kwa wao. Hata hivyo Trump hakuonesha uungwaji mkono wowote kwa Kevin McCarthy.

Ikulu ya Marekani imewahimiza wabunge wa nchi hiyo kuharakisha mchakato wa kumpata spika mpya wa Baraza la Wawakilishi. Msemaji wa Ikulu ya White House Karine Jean-Pierre amesema rais Joe Biden angependelea kuona spika mpya anapatikana bila mivutano ili bunge lirudi kazini kushughulikia changamoto zinazolikabili taifa hilo.

Mbunge Patrick McHenry wa Republican, ambaye alimuunga mkono Kevin McCarthy, sasa ndiye Spika wa muda. Aliiweka Bunge kwenye mapumziko. 

Vyanzo: Reuters, AFP, AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW