1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khamenei asema Jamhuri ya Kiislamu ni mti usiotikisika

15 Oktoba 2022

Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, amesema hakuna mtu anayepaswa kufikiria wanaweza kuiondoa Jamhuri ya Kiislamu ya nchi hiyo katika onyo kali kwa waandamanaji

Ayatollah Ali Khamenei
Picha: IRANIAN LEADER PRESS OFFICE/AA/picture alliance

 

Katika matamshi yake yaliopeperushwa katika televisheni ya taifa, Khamenei amesema kuwa mche huo ambao ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mti mkubwa sasa na hakuna mtu anayepaswa kuthubutu kufikiria wanaweza kuung'oa.

Maandamano ya watu kutoka matabaka mbali mbali baada ya kifo cha Mahsa Amini, mwanamke wa Kikurdi aliyefariki chini ya ulinzi wa polisi kufuatia kukamatwa kwake kutokana na kile kilichotajwa kuwa mavazi yasiyofaa, yamebadilika kuwa wito wa kuondolewa kwa Khamenei na kile kilichoitwa kifo kwa Jamhuri ya Kiislamu.

Maandamano nchini Iran changamoto kubwa kwa utawala

Maandamano hayo yanaashiria mojawapo ya changamoto kubwa zaidi kwa utawala wa kidini nchini humo tangu mapinduzi ya 1979, hata kama machafuko hayo hayaonekana kuwa karibu kuiangusha serikali.

Baadhi ya machafuko mabaya zaidi yamekuwa katika maeneo yenye makabila madogo ambayo yamekuwa na malalamiko ya muda mrefu dhidi ya serikali,  ikiwa ni pamoja na Wakurdi katika eneo la Kaskazini-Magharibi na Wabaluchi katika eneo la Kusini Mashariki.

Maandamano nchini Iran kufuatia kifo cha Mahsa AminiPicha: UGC

Iran imesema ghasia hizo zimesababishwa na maadui ndani na nje ya nchi, yakiwemo  makundi yaliojihami yanayotaka kujitenga pamoja na mataifa ya Magharibi. Mamlaka ya Iran imekanusha kuwa vikosi vya usalama vimewauwa waandamanaji. Televisheni ya serikali imeripoti kuwa takriban maafisa 26 wa vikosi vya usalama wameuawa.

Amnesty International yasema watoto 23 wamekufa

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema zaidi ya watu 200 wameuawa kutokana na ukandamizaji, ikiwa ni pamoja na wasichana wadogo. Amnesty International imesema takriban watoto 23 wamekufa.

Kifo cha Amini na ukandamizaji huo umelaaniwa na Marekani na mataifa mengine ya Magharibi, na kusababisha vikwazo vipya kwa maafisa wa Iran na pia kuongeza mvutano katika wakati ambapo mazungumzo ya kufufua mkataba wa nyuklia wa 2015 yamekwama.

Iran yenye idadi ya watu milioni 87, ni makazi ya makabila saba madogo pamoja na Waajemi walio wengi. Makundi ya haki yanasema walio wachache, wakiwemo Wakurdi na Waarabu, kwa muda mrefu wamekabiliwa na ubaguzi, jambo ambalo Iran inakanusha.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW