1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khan aongoza huku uhesabuji kura ukicheleweshwa Pakistani

Yusra Buwayhid
26 Julai 2018

Zoezi la kuhesabu kura lililocheleweshwa limezua fujo na madai ya udanganyifu katika uchaguzi wa Pakistani. Baadhi wameyakataa matokeo kabla ya hata kutangazwa. Nyota wa zamani wa kriketi Imran Khan anaonekana kuongoza.

Pakistan Wahl | Anhänger von Imran Khan, Tehreek-e-Insaf-Partei
Picha: Reuters/A. Perawongmetha

Wakiwa barabarani, wafuasi wa chama cha Tehreek-e-Insaf (PTI) cha mchezaji wa zamani wa kriketi Imran Khan wanaonekana wakishangilia ushindi wa mgombea wao ingawa ni asilimia 48 tu ya kura ambayo tayari zimeshahesabiwa hadi sasa, kutokana na kucheleweshwa kwa zoezi hilo.

Tume ya Uchaguzi ya Pakistani (ECP) imesema, mchakato wa kuhesabu kura umecheleweshwa kutokana na sababu za kiufundi, huku ikikataa madai ya udanganyifu. Katibu wa tume hiyo, Babar Yakoob, aliviambia vyombo vya habari siku moja baada ya uchaguzi kwamba kuchelewa huko kumetokana na kuharibika kwa mfumo wa utoaji matokeo wa (RTS). Ni programu ya simu ya mkononi, ilioanza kutumiwa kwa mara ya kwanza katika uchguzi huo, ili kuhesabu kura na kutoa matokeo kutoka zaidi ya vituo vya kupigia kura 85,000.

Katika juhudi za kutaka kutuliza fujo lilozuka nchini humo, Katibu wa tume hiyo ya uchaguzi Babar Yakoob alijaribu kuidhibiti hali kwa kusema tume yake itatangaza chochote kile kitakachoendelea.

"Mara moja nimekuja hapa kulishuhudia mwenyewe suala hili muhimu, ili kusitokee mjadala wowote bila sababu muhimu. Baadae kutakuwa na maendeleo zaidi juu ya suala hili," amesema Yakoob.

Vyama vikuu vyadai udanganyifu wa uchaguzi

Wafuasi wa Imran Khan wakishangilia kabla ya utangazaji wa matokeo kukamilikaPicha: Getty Images/A.Ali

Masaa machache baada ya zoezi la kupiga kura kukamilika Jumatano, vyama vikuu vya kisiasa nchini humo vilidai uchaguzi ulikuwa na udanganyifu kabla ya hata matokeo kuanza kutangazwa. Chama cha waziri mkuu wa zamani aliyefungwa jela Nawaz Sharif, kimelishutumu jeshi la nchi kuhusika katika udanganyifu huo.

Soma zaidi: Wapakistan wamaliza kupiga kura licha ya mashambulizi na mauaji

Kulingana na matoke yasiyo rasmi yaliyotangazwa na vyombo vya habari vya ndani ya nchi, chama cha Tehreek-e-Insaf (PTI) cha Khan ambacho kinadaiwa kuungwa mkono na jeshi hilo, kimepata asilimia kubwa ya kura huku chama cha Sharif kikiwa kimeshika nafasi ya pili.

Zaidi ya watu milioni 105 wamesajiliwa kupiga kura katika uchaguzi huo wa viti 849 vya bunge la taifa na mabunge ya majimbo. Wagombea zaidi ya 11,000 wanachuana katika kinyanga'nyiro hicho.

Wanajeshi na maafisa wa polisi wapatao 800,000 walisambazwa, ili kuhakikisha usalama wa nchi siku ya uchaguzi. Lakini bado uligubikwa na mashambulizi. Shambulio kubwa la bomu lilodaiwa kufanywa na kundi linalojiita Dola ala Kiislam IS, lilisababisha vifo vya watu 31 na 70 kujeruhiwa karibu na kituo cha kupigia kura cha Quetta, kusini-magharibi mwa jimbo la Balochistan.

 

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/afr/dpa

Mhariri: Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW