KHARTOUM: Maofisa na waandishi habari wa Marekani watendewa ubaya mjini Khartoum
21 Julai 2005Matangazo
Maofisa na waandishi habari wa Marekani wametendewa ubaya na walinda usalama wa Sudan mjini Khartoum. Tukio hilo lilifanyika wakati waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice alipokuwa akifanya mazungumzo na rais wa Sudan, Omar el-Bashir. Waandishi na maofisa hao wamesema maofisa wa usalama waliwazuia kuingia kwenye mkutano huo na kusukumwa.
Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Marekani amesema wizara ya mambo ya kigeni ya Sudan imeomba msamaha kwa kisa hicho. Hapo awali Condoleezza Rice alisisitiza msimamo wa serikali yake kwamba vita katika eneo la Darfur vimesababisha mauaji ya halaiki.