1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khartoum. Serikali ya Sudan ina matumaini ya kupata fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi mpya kusini mwa nchi hiyo.

10 Aprili 2005

Serikali ya Sudan imesema inamatumaini kuwa fedha za kutosha zitapatikana katika mkutano wa wafadhili utakaoanza Jumatatu kwa ajili ya ujenzi mpya wa eneo la kusini mwa nchi hiyo lililokumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda wa miaka 21.

Waziri wa mambo ya kigeni Bwana Moustafa Osmane Ismail amewaambia waandishi wa habari kuwa anatarajia mkutano huo wa siku mbili unaoanza mjini Oslo kesho Jumatatu utakuwa wa mafanikio, licha ya juhudi za baadhi ya makundi kuitumia hali ya jimbo la Dafur kuweza kuwa na matokeo mabaya kwa mkutano huo.

Wito wa kupatikana kwa fedha za ujenzi mpya umekuja baada ya serikali ya Sudan na jeshi la waasi wa kusini mwa nchi hiyo la SPLM, kutia saini makubaliano ya amani mwezi Januari na kumaliza miongo miwili ya mapigano.

Wakati huo huo Sudan imesema itaondoa vizuizi kuhusiana na nyendo za wanadiplomasia wa Marekani nchini humo, hatua iliyowekwa kulipiza hatua kama hiyo iliyowekwa na Marekani dhidi ya wanadiplomasia wa Sudan. Waziri wa mambo ya kigeni amesema kuwa hatua hiyo itaondolewa siku ya Jumatatu.

Nayo Peru imesema kuwa itashiriki katika jeshi la umoja wa mataifa la kulinda amani nchini Sudan na Ivory Coast kwa muda wa mwaka mmoja. Serikali ya Peru imetangaza jana kuwa itawatuma maafisa saba wa kijeshi nchini Sudan wiki hii kujiunga na ujumbe wa umoja wa mataifa wa kulinda amani nchini humo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW