KHARTOUM : Umoja wa Afrika kutuma vikosi zaidi Dafur
25 Septemba 2006Umoja wa Afrika unapanga kupeleka vikosi zaidi nchini Sudan kuimarisha shughuli zake za kulinda amani huko Dafur jimbo lililoathiriwa na mapigano magharibi mwa Sudan.
Hatua hiyo inakuja wakati shinikizo la kimataifa likiongezeka kutaka Sudan kuruhusu kikosi cha Umoja wa Mataifa cha wanajeshi 20,000 kuchukuwa nafasi ya kikosi cha wanajeshi 7,000 wa Umoja wa Afrika kiliopo hivi sasa ambacho kinakabiliwa na ukata wa kukigharamia huko Dafur.
Msemaji wa Umoja wa Afrika Nouredine Mezni amesema itakuwa ni suala la vikosi na kwamba hawezi kuainisha itakuwa vikosi vingapi lakini amesema kimsingi wataongeza idadi ya wanajeshi wake.
Kwa kawaida kikosi kimoja huwa na wanajeshi 600 hadi 800.
Wakati wataalamu wa misaada wakitabiri maafa mapya ya kibinaadamu huko Dafur iwapo wanajeshi hao wa Afrika wataondolewa Umoja wa Afrika ulikubali wiki iliopita kuongeza mamlaka ya shughuli zake hadi tarehe 31 mwezi wa Desemba baada ya muda wake kumalizika hapo tarehe 30 Septemba kwa msaada wa Umoja wa Mataifa na mataifa ya Kiarabu.