KHARTOUM : Umoja wa Afrika wataka ushirikiano na waasi
11 Juni 2007Matangazo
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika walioko huko Dafur nchini Sudan wametowa wito wa kuwepo ushirikiano mzuri kati ya wanajeshi wake na waasi wa zamani ambao hivi sasa wamejiunga serikali ya Sudan lakini wamedai waasi hao wayarudishe magari yao 12 waliopora.
Jeshi la Sudan na washirika wao wanamgambo wanaojulikana kama janjaweed wanashutumiwa kwa kiasi kikubwa kwa umwagaji mkubwa wa damu dhidi ya raia ambapo watu 200,000 wameuwawa na wengine milioni mbili na nusu kupotezewa makaazi katika kipindi cha miaka minne ya mapigano katika jimbo hilo.
Hata hivyo makundi mbali mbali ya waasi yanalaumiwa kwa vitendo vingi vya utekaji nyara ambavyo hukwamisha vibaya juhudi za wafanyakazi wa misaada kwenye jimbo hilo.