KHARTOUM : Waarabu watakiwa wasaidie Umoja wa Afrika huko Dafur
5 Juni 2005Sudan imezitaka nchi za Kiarabu hapo jana kusaidia juhudi za Umoja wa Afrika kuleta utulivu katika jimbo lake la magharibi la Dafur lililokumbwa na vita ambalo ni eneo la maafa makubwa ya kibinaadamu.
Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Mustafa Osman Ismail ameushukuru Umoja wa Waarabu kwa mchango mzuri katika jitihada zinazotumika kushughulikia mgogoro wa Dafur.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari wa pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Waarabu Amr Mussa aliyoko ziarani Sudan Ismail amesema wanasubiri kwa hamu msaada wa moja kwa moja wa Waarabu kwa Umoja wa Afrika na wanajeshi wa kulinda amani wa umoja huo huko Dafur.
Wanajeshi wa Umoja wa Afrika wanasimamia usitishaji lege lege wa mapigano kati ya serikali ya Khartoum na waasi wa kabila la wachache huko Dafur na wiki iliopita wafadhili wa kimataifa wameahidi takriban dola milioni 292 kwa ajili ya msaada zaidi kwa shughuli za kulinda amani za Umoja wa Afrika.